Aliwasili nchini Machi 5, 1990 na kulakiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa Dar es Salaam (Sasa Uwanja wa Julius Nyerere) na Mwalimu
Nyerere.
Baada ya kuwasili, alikagua gwaride kama ilivyo kawaida, lakini kikubwa
ilikuwa ni hamasa ya Watanzania hasa wakazi wa Dar es Salaam na
vitongoji vyake, maelfu kwa maelfu kujipanga barabarani kumlaki kiongozi
huyo katika njia zote alizopita kuanzia Uwanja wa Ndege.
Pamoja na mvua za masika zilizokuwa zinanyesha, hakuna aliyejali hali hiyo. Kila mmoja alikuwa na shauku ya kumwona Mandela.
Ilielezwa kuwa Mandela na ujumbe wake angewasili mapema zaidi, saa 4:00
asubuhi, lakini ratiba ilibadilika kuwa angewasili saa 11 jioni, lakini
watu hawakupungua barabarani, walijipanga mapema kuanzia Uwanja wa
Ndege, Barabara ya Pugu (sasa Nyerere) na maeneo mengine kumlaki
mpigania uhuru huyo.
Wakati huo Dar es Salaam ilikuwa na tatizo kubwa la usafiri, lakini hakuna aliyejali. Marabaada ya Mandela kutua, ilinyesha mvua kubwa, watu walikubali kulowa lakini hadi wamwone Mandela.
Mandela alipata mapokezi makubwa na ya aina yake jijini Dar es Salaam.
Kikubwa ni kwamba, Mandela alikuwa akizungumzwa sana na vyombo vya
habari, kuonwa kwenye magazeti lakini wengi walitaka kumwona Mandela na
mkewe Winnie uso kwa uso.
Baada ya shughuli za Uwanja wa Ndege kukamilika na mvua kukatika,
Mandela aliyefuatana na mkewe, Winnie walipanda gari ya wazi aina ya Rolls Royce wakiwa na Mwalimu Nyerere kwa pembeni.
Maelfu kwa maelfu ya wakazi wa Dar es Salaam walijipanga kuanzia Uwanja
wa Ndege, Barabara ya Pugu, Uhuru, Kariakoo, Stesheni, Luthuli hadi
Ikulu na watu wote hao walikuwa na shauku ya kumuona Mandela walitimiza
kiu yao. Kila mmoja alifurahi baada ya kumuona Mandela aliyekuwa
akipunga mkono muda wote.
“Ndoto yangu imetimia”, “Siamini, nimemwona Mandela?”, “Safi”, “Naweza
kufa kwa amani...nimemwona Mandela” zilikuwa kauli za watu mbalimbali
waliokuwa wamejipanga barabarani kumlaki Mandela akiwa na Winnie
walipokuwa wakipita.
Siku iliyofuata, hali ilikuwa zaidi ya siku ya mapokezi. Watu waliombwa
kufika kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) na ilikuwa mminyano
wa aina yake. Zaidi ya watu 100,000 wanasadikiwa walifurika uwanjani
kusikiliza hotuba ya pili ya Mandela tangu atoke gerezani.
Mandela alitoa hotuba ya kwanza akiwa City Hall nchini Afrika Kusini.
Aliwahutubia wafuasi wa ANC wapatao 50,000 waliokuwa wakimsubiri kwa
hamu kumuona baada ya kifungo cha miaka 27 jela, ambako pamoja na yote
alionyesha furaha yake kulakiwa na maelfu ya wapenzi na wafuasi wake
hao.Mwalimu Nyerere akiwa na mgeni wake, alianza kumpongeza Mandela kwa
kuwa ni kati ya watu wanaostahili heshima kutokana na mapambano yake
dhidi ya siasa dhalimu ya makaburu wa Afrika Kusini. Makaburu
walikithiri kwa siasa zao za kibaguzi.
Alisema kuwa kujitokeza kwa watu wengi kiasi hicho ilikuwa inadhihirisha
kuwa Mandela anagusa akili za watu wengi kutokana na mapambano ya
kumtetea mtu mweusi.
Kutokana na mchango wake wa kupigania haki na uhuru, Mwalimu Nyerere alimtunukia Mandela, Nishani ya Kilimanjaro Daraja la Pili ambayo mara nyingi hupewa Mawaziri Wakuu na viongozi wengine wenye kariba kama ya Mandela.
Akihutubia maelfu ya Watanzania na sauti yake nzito, Mandela alionyesha furaha yake kwa mapokezi makubwa ya Watanzania.
Pia Mandela alitumia nafasi hiyo kuwashukuru Watanzania kwa kukiunga
mkono chama chake cha ANC katika mapambano ya ukombozi dhidi ya ubaguzi
na utawala dhalimu wa makaburu.
Ziara ya Zanzibar
Machi 7, 1990 ujumbe wa Mandela ulikwenda Zanzibar ambako pia shughuli
mbalimbali zikiwamo za biashara zilisimama kwa takribani saa nne, huku
kila mmoja akiwa na shauku ya kumuona Mandela.
Mbali na kufurika mitaani, Uwanja wa Ndege ulikuwa umefurika pamoja na
Uwanja wa Uwanja wa Amaan, Wazanzibar walijaa kumlaki ‘Comrade’ Mandela.
Neno ‘Amandla’ lilisikika kutoka kwa waliofika kumlaki Mandela aliyekuwa
amepakizwa kwenye gari aina ya Landrover kwenda uwanjani.
Itakumbukwa, kwa mara ya kwanza, Mandela na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Karume, walikutanaAddis Ababa mwaka 1962.
Mandela aliyetembelea Tanzania kwa mara ya kwanza katika ziara fupi
mwaka 1962, alipofika Zanzibar baada ya kutoka gerezani, aliomba
apelekwe kwenye Kaburi la Karume pamoja na eneo ambalo Rais Karume
aliuawa.
Kati ya vitu alivyovizungumza akiwa Zanzibar, alisifu Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar na kwamba viongozi wa Afrika wanaosaka umoja,
wajifunze muundo huo wa Muungano kutoka Tanzania.
No comments:
Post a Comment