KIBURUDANI
na kimahudhurio Tamasha la Gurumo 53 lililofanyika Jumamosi TCC Club
lilifana sana, lakini likazungukwa na majaribu mengi yaliyotia doa.
Waliokuwa
wakihisi kuwa itakuwa ni burudani mwanzo mwisho wala hawakukosea,
ndivyo ilivyokuwa pale muziki ulipoanza kulia saa 4 na nusu za usiku –
ikawa ni burudani mwanzo mwisho.
Mpangilio
wa ratiba ya utumbuizaji ulikuwa mzuri sana, MC Masoud Masoud alimudu
vema eneo lake na kuonyesha weledi wa hali ya juu.
Ilikuwa
kumbukumbu inayoweza kukutoa chozi pale wanamuziki wengi wakongwe
walipojitokeza na kushiriki kutumbuiza katika tamasha hilo.
Twanga Pepeta jukwaani
Nyimbo
kama “Vicky” na “Tulizaliwa wote Kijiji kimoja” za Komandoo Hamza
Kalala akiwa na bendi za Bantu Group na UDA Jazz zilikuwa ni miongoni
mwa burudani kali ambazo kamwe hazitahaulika katika usiku ule.
Hussein Jumbe hakubahatisha
Komandoo Kalala na mwanae Kalala Jr wakitesa jukwaani
Mzee
Makassy anayepiga muziki wa kiroho nae akapanda jukwaani na
kuwakumbusha watu enzi za Makassy Orchestra kwa kupiga wimbo wake wa
“Anifa” ambao ulisisimua sana kiasi cha baadhi ya mashabiki kupiga
kelele wakitaka wimbo urudiwe.
Miraji Shakashia, mmoja wa wanamuziki waliofunika sana
Aliyefanya
watu wakusanyike kwa usiku ule, Muhidin Maalim Gurumo akapanda jukwaani
akiwa amepiga suti ya kahawia na kutumbuiza kwa saa nzima bila
kupumzika.
Alishiriki kwenye nyimbo kama “Selina” na “Gama” za Sikinde, “Chatu” wa Ndekule pamoja na nyimbo kadhaa za Msondo.
Licha
ya kuwa nje ya ulingo kwa muda mrefu kutokana na kuugua, Gurumo alipiga
kazi ya kufa mtu, ubora wa sauti yake ulikuwa pale pale na hata sekunde
moja hakutoka nje ya ufunguo.
Wadau wa kundi la Bongo Dansi nao walikuwepo
King Maluu aliteka hisia za mashabiki
Kwa
hakika ilikuwa ni burudani ya kukata na shoka, umati wa mashabiki wa
muziki wa dansi walifurika kwa wingi katika viwanja vya TCC Club
Chang’ombe.
Hata
hivyo licha ya utamu wote huo, tamasha liliingia dosari kubwa la
hitilafu ya vyombo, hali iliyopelekea baadhi ya mashabiki kumaliza akiba
yao yote ya ustaarabu.
KOSA LA KWANZA:
Waendeshaji
wa viwanja vya TCC Club wakijua wazi kuwa wameukodisha uwanja kwaajili
ya tamasha la Gurumo, wakaukodisha pia kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania.
Bandari wakawa na bonanza lao michezo ambalo liliisha saa 12.30.
Jukwaa
la tamsha la Gurumo ambalo lilipaswa kufungwa kwenye uwanja wa soka
ikabidi lifungwe sehemu nyingine kwa vile Bandari walikuwa wanautumia
uwanja huo.
KOSA LA PILI:
Baada
ya jukwaa kukamilika pamoja na ufungaji wa vyombo vya kisasa, yalipaswa
kufanyika majaribio ya sauti, lakini hilo lilichelewa sana.
Kuanzia
saa 1 usiku tayari kila kitu kilikuwa kimekamilika jukwaani lakini
waendeshaji wa vyombo hivyo walioletwa na Clouds FM kama sehemu ya
udhamini, walijizungusha zungusha na hadi ilipofika saa 2.30 usiku.
Ni
katika muda huo ndipo walijaribu kuwasha mitambo yao lakini kukatokea
hitilafu ya umeme iliyopelekea baadhi ya vyombo vyao kuathiriwa na
kushindwa kufanya kazi.
KOSA LA TATU:
Baada
ya kutokea tatizo hilo, bado waendeshaji wa vyombo hivyo walikaa kimya
huku wakishika hiki na kile bila kuwaeleza waandaji nini kinachoendelea.
Baada
ya waandaji kushtushwa na ukimya wa muda mrefu ndipo waliposegea eneo
la jukwaa na kuwaambia sasa MC anahitaji kupanda jukwaani na kufungua
rasmi onyesho, lakini wakakutana na majibu ya utata. Hiyo ni saa 3
usiku.
“Vyombo vyetu vimeungua, fundi umeme wa ukumbi katuunguzia busta, hapa muziki haulii tena,” alisema mmoja wa mafundi mitambo.
“Hii ni show ya msaada tu, ina thamani gani kwetu mpaka ituunguzie vyombo vyetu,” aliongeza.
Hata
baada ya kubembelezwa sana na kuambiwa kwa kawadia si rahisi busta zote
kuungua kwa wakati mmoja hivyo waendelee na busta zilizo salia, bado
waligoma. Saa 4 usiku hiyo.
Kama
ni kweli vyombo vyao viliungua au vilishindwa tu kufanya kazi na kisha
wakaamua kusingizia mambo ya umeme, hiyo ni siri yao, hawakutaka ukaribu
na mtu yeyote.
MSONDO WAOKOA JAHAZI:
Baada ya vyombo vya Clouds kugoma kazi, vyombo vya Msondo Ngoma Music
Band viletwa na kufungwa kwa haraka haraka na ilipotimu saa 4.30 vyombo
vikanguruma jukwaani, show ikaanza, amani ikarejea na watu wakasahau
maudhi yote.
Ni wazi kuwa makosa hayo matatu yangedhibitiwa na kila kitu kwenda na wakati kama kilivyopangwa basi onyesho lisingeingia doa.
TCC wasingeutoa uwanja kwa watu wa Bandari, maana yake jukwaa lingefungwa mapema zaidi.
Jukwaa lingefungwa mapemba maana yake ni kwamba vyombo vingejaribiwa mapema.
Kama vyombo vingejaribiwa mapema, tatizo la umeme kuunguza vyombo lingetokea mapema na suluhisho lingepatikana mapema.
ILIKUWEJE FUJO ZIKAIBUKA?
Wakati vyombo vya Clouds vikizingua na muda ukiwa unasogea kwa kasi, baadhi ya mashabiki uzalendo ukawashinda.
Wakaanza kutukana, wengine wakaenda magetini kudai viingilio vyao, wengine wakafanya fujo na wengine wakitoka na vitu.
Hali
hiyo ikapelekea watu waliokuwa wakilinda getini kuingia mitini, mageti
yakabaki wazi, watu wakaingia na kutoka bila kizuizi.
Hali hiyo ilidumu hivyo hadi pale muziki ulipoanza kulia ndipo utulivu ukarejea na kila mtu kurudi kwenye eneo lake.
CREDIT : SALUTI 5
No comments:
Post a Comment