14 November 2013

ZITTO AFICHUA KASHFA NZITO TUME YA UCHAGUZI TANZANIA


TUME ya Uchaguzi nchini (NEC) inadaiwa kuingia katika mchakato wa mwisho wa kuzipa zabuni ya kuandaa vifaa vya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kampuni za M/S Jazzmatrix Cooperation na M/S Invu IT Solution zinazodaiwa kuwa na rekodi mbaya ya utendaji.

Tanzania Daima limedokezwa kuwa mkakati huo unahusishwa na  njama za kutaka kukibeba Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi huo kwa kuchakachua matokeo ya kukibakiza madarakani.


 Kampuni hizo ambazo katika zabuni ya Tume ya Uchaguzi zimetajwa kushirikiana na Kampuni ya Kitanzania ya M/S SCI Tanzania Limited, mbali ya kutojulikana zinapotoka, pia ndizo zimekuwa na gharama kubwa kuliko kampuni nyingine zilizoomba kazi hiyo.

Kiwango ambacho kampuni hizo zilitaja na kukubaliwa na NEC kwa ajili ya kuandaa vifaa vya kielektroniki vya kusajili wapiga kura (Biometric Voters Registration) ni zaidi ya euro milioni 60, sawa na sh bilioni 126.3, wakati kampuni zinazofuata zikihitaji kuanzia euro milioni 40.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, ni mmoja wa viongozi waliofichua mkakati huo, akidai unafanywa na serikali ya CCM ili kuhakikisha wanajiandaa kudhibiti kila eneo ili waweze kubaki madarakani.

Alisema lengo ni kuhakikisha mchakato wa vitambulisho vya kupigia kura vya kielektroniki vina kuwa na faida kwa CCM na kukiingizia fedha chama hicho za kutumia kwenye uchaguzi huo kupitia mfumo huo dhaifu wa vitambulisho hivyo.

Zitto alisema kutokana na hali hiyo, amemwandikia Mdhibiti na Mkaguzi  Mkuu wa Serikali (CAG) barua ya kutaka ukaguzi wa zabuni hiyo ufanyike kwa kushirikisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na vyombo vingine vya usalama kwa ajili ya kujiridhisha.

“Wenzetu CCM wanafanya mikakati ya kujiandaa na Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kuhakikisha wanapata fedha za kutosha na hata mazingira mabaya ya vifaa vitakavyotumika katika upigaji kura na sasa wameshaingia hata katika Tume ya Uchaguzi kwa ajili ya kutengeneza mazingira,” alisema Zitto.

Aliongeza kuwa kiasi kilichotolewa ni kodi ya Watanzania na kwamba ni vema taifa likajiridhisha kuwa matatizo yaliyotokea Kenya na Ghana hayatajirudia Tanzania, hasa wakati wa upigaji kura.

 Gazeti hili limeona barua hiyo ya Zitto kwenda kwa CAG, ya Novemba 7, 2013, yenye kichwa cha habari; ‘Zabuni ya  Biometric Voters Registration (BRV KITS) No. IE/018/2012-13/HQ/G/19 yenye thamani ya sh bilioni 126.3.’

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini anasema kuwa  NEC imekuwa katika mchakato wa zabuni tajwa hapo juu.

“Zabuni hiyo sasa imeanza kuleta malalamiko miongoni mwa wananchi kutokana na kinachosemekana kuwa kampuni iliyopewa zabuni hiyo haina uwezo kiteknolojia, pia bei zao ni kubwa.

“Katika mafunzo ya hivi karibuni ya SADCOPAC jijini Nairobi tuliazimia kuwa ni vema kwenye zabuni nyeti kama za namna hii, SAIs wawe na uwezo wa kufanya ukaguzi kabla ya zabuni kutolewa na kuanza kutekelezwa,” alisema.

Kwa mujibu wa nyaraka za NEC ambazo Tanzania Daima linazo, kampuni zilizopewa tenda ya pamoja yenye kugharimu kiasi cha dola 78, 987,636.00, sawa na sh 126,291,375,455 ni M/S Jazzmatrix Cooperation na M/S Invu IT Solution ambazo hazijulikani nchi zinapotoka zikiwa zinashirikiana na M/S SCI Tanzania Limited.

 Katika nyaraka hizo kampuni zilizokosa tenda na ambazo zimelalamika kwa Mkurugenzi wa NEC namna mchakato wa kutoa zabuni hiyo ulivyoendeshwa zimeainishwa kuwa ni M/S Zetes SA ya nchini Ubalgiji, M/S IRIS Corporation Technology ya Malaysia, M/S Lithotech Exports ya Afrika Kusini, M/S Safran Morpho ya Ufaransa na  M/S Avante International Technology, Inc ya Marerkani.

 Kampuni hizo zinahoji njia na sababu zilizowafanya wakose tenda hiyo licha ya kuwa na uzoefu, vifaa bora pamoja na kuwa na kiwango kidogo cha gharama tofauti na kampuni iliyopewa kazi.

 Katika moja ya malalamiko yao, Kampuni ya M/S Morpho, inalalamika kutofahamishwa namna walivyokosa vigezo vya kupata kazi hiyo licha ya kuwa na sifa za kimataifa za kufanya kazi huku ikiwa imetoa bei nafuu kuliko kampuni iliyopata kazi.

 “Tulikuwa miongoni mwa washindani muhimu kwa kuwa kiwango chetu kilikuwa ni sh bilioni 97.8 ambazo ni sawa na euro 44,939,912 + sh 3,843,736,140.

“Ujuzi, vigezo na uzoefu wetu havilingani, duniani kote tumefanya kazi katika maeneo mengine kwa ufanisi na tunashindwa kuelewa kivipi walishinda hao ambao wamepata kazi kwa kiwango cha zaidi ya sh bilioni 27.8 ikilinganishwa na yetu,” ilisomeka sehemu ya barua.

 Alipotafutwa Mkurugenzi wa NEC, Julius Mallaba, alisema hawezi kuliongelea suala hilo katika simu na kuomba mwandishi awasiliane na Kaimu Mkurugenzi wa NEC, Dk. Sist Cariah, ambaye alisema mchakato wa kupata kampuni ulifuatwa kisheria.

Dk. Cariah alisema si kweli kwamba kampuni iliyopewa kazi haina uwezo bali malalamiko yanatoka kwa watu walioshindwa kupata kazi hiyo.

Alipoulizwa juu ya uzoefu wa kampuni hiyo na wapi ilifanya kazi, Dk. Cariah alisema kwa maelezo waliyonayo ni kwamba kampuni hiyo ina uzoefu wa miaka 35 wa kufanya kazi, huku akishindwa kuainisha sehemu ilizowahi kufanya kazi.

Kuhusu wapi zimetoka kampuni hizo, Dk. Cariah alisema suala la kutoainishwa kimaandishi ni makosa ya kawaida, huku akitaja kuwa zinatoka katika nchi ya India na Australia.

Kuhusu gharama, Dk. Cariah alisema licha ya makampuni mengine kutaja gharama za chini, zingeweza kuwa na gharama kubwa zaidi wakati wa kukamilisha kazi hiyo kutokana na kuwa na gharama zilizojificha.

Chanzo :Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname