Dodoma: Wabunge Wawili Maarufu wa
Chadema, Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini) na Godbless Lema (Arusha Mjini)
wameingia katika vita ya maneno ambayo chanzo chake ni kauli ya Lema
aliyotoa katika kikao cha wabunge (briefing) kilichofanyika mjini Dodoma
Jumanne wiki hii.
Lema akizungumza katika kikao hicho,
anadaiwa kutoa maneno ambayo yalitafsiriwa na wabunge wengi kuwa
yalikuwa yakimlenga Zitto kuhusu hatua yake ya kukataa posho na
kumtuhumu kwamba ana ukwasi ambao unapaswa kuhojiwa.
Gazeti hili lilimtafuta Lema likirejea
taarifa iliyotolewa na Zitto akilalamika kwamba Lema alimshambulia
katika kikao hicho cha wabunge wote na kwamba alikuwa akimlenga yeye.
Lema, hata hivyo, alikiri kuzungumzia suala hilo akisema:
“Mimi sikumtaja mtu, kwahiyo kama kuna mtu analalamika hilo ni suala jingine, ila mimi nilimaanisha nilichokisema”.
Hata hivyo, Zitto alieleza kuwa msimamo
wa Lema ulikuwa unapingana na wabunge wengine wa Chadema, ambao waliwahi
kupendekeza kuwa posho zifutwe.
Zitto alisema kuwa yeye mwenyewe, Mbunge
wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika
waliwahi kupendekeza kuwa posho zifutwe.
“Mimi sipokei posho kabisa, posho za
vikao na ndiye mbunge pekee ambaye hapokei posho ya vikao tangu mwaka
2011,” aliongeza Zitto, ambaye anahudhuria mkutano unaozungumzia
uendeshaji wa Serikali kwa uwazi huko London, Uingereza.
Zitto alisema malipo ya wabunge mpaka
sasa ni makubwa sana ukilinganisha na hali ya wananchi wakati Serikali
ikishindwa kulipa vizuri walimu na wauguzi.
“Hatuwezi sisi kama wabunge kuanza
kulilia posho, wakati wananchi wetu hawana maji, hatuwezi kulilia posho.
Mbunge anayetaka posho zaidi akafanye kazi nyingine na awaachie
wanaoweza kuwakilisha watu waendelee,” alisema Zitto.
Lema, hata hivyo, alisema kwamba katika
mkutano huo aliweka bayana kwamba umasikini siyo uzalendo na kusisitiza
kuwa wabunge wanapaswa kuwa na maslahi bora na wakati huohuo wana wajibu
wa kuwatetea watumishi wengine wa umma.
“Nilisema huwezi kuzuia taasisi moja
kupewa maslahi bora eti tu kwa sababu watumishi wengine hawalipwi
vizuri, ni haki wabunge kulipwa vizuri na wakati huo wapiganie maslahi
ya watumishi wengine,” alisema Lema na kuongeza:
“Kwahiyo nikasisitiza kwamba nawashangaa
wale ambao wanakataa posho ya Sh80,000 na ukienda kuchunguza wanakatwa
fedha zote kutokana na mikopo waliyochukua, lakini bado wakija sehemu
kama Arusha wanalala kwenye hoteli ya gharama kubwa kati ya Dola za
Marekani 150 na 600”.
Alisema katika mazingira hayo kunakuwapo
maswali mengi yasiyokuwa na majibu na kwamba mbunge wa aina hiyo
alitakiwa anapokuwa katika mji wowote nchini aishi katika hoteli yenye
thamani kati ya Sh20,000, 30,000 na hata Sh50,000.
“Kwa hiyo ikiwa unakataa posho ya
Sh80,000 halafu unalala chumba cha Dola 600 hustahili kupata credibility
(sifa) stahili, ni unafiki tu na kutafuta sifa za kipuuzi,”alisema
Lema.
Alisisitiza kwamba wabunge wa Tanzania
hawalipwi ipasavyo na kwamba kudai malipo ya ziada hakuwaondolei wajibu
wao wa kuwatetea watumishi wengine wa umma ambao pia malipo yao ni
kidogo.
“Kuna hatari ya kuona kwamba Sh80,000 au
Sh200,000 ni fedha nyingi, ni kwamba kama sisi wabunge tutalipwa
Sh50,000 basi maana yake ni kwamba walimu au polisi tutaridhika
wakilipwa hata Sh10,000,”alisema
No comments:
Post a Comment