26 November 2013

Mwili wa Mtanzania Aliyeuawa Nchini Kenya wawasili Nchini...!!



MWILI wa mwanafunzi Mtanzania Jerry Mruma (23) aliyeuawa Nairobi nchini Kenya, umewasili nchini jana na kupokelewa na ndugu, jamaa na marafiki katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.

Jerry aliyekuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Marekani (USIU) tawi la Nairobi, aliuawa nchini humo mwishoni mwa wiki iliyopita na anatarajiwa kuzikwa leo katika makaburi ya Kinondoni.

Kabla ya maziko, ratiba ya mazishi inaonesha kuwa kutakuwa na ibada itakayofanyika saa 7.00 mchana katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Usharika wa Mbezi Beach, lililopo eneo la Tangi Bovu.

Baadhi ya ndugu jamaa na marafiki waliojitokeza kupokea mwili huo, walibubujikwa machozi wakati walipokuwa wakitoa pole kwa wazazi pamoja na wanafamilia wengine, akiwepo kaka wa marehemu Khan na mdogo wake Kelvin.

Marehemu ni mtoto wa aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa Tanzania Standard Newspapers (TSN), wachapishaji wa magazeti ya Daily News, Sunday News, HabariLeo, HabariLeo Jumapili na SpotiLeo Isaac Mruma.

Jerry mbali na kuwa mwanafunzi, pia alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Kilimo Yetu jijini Nairobi, inayojishughulisha na masuala ya kilimo.

Kaimu Mhariri Mtendaji wa TSN, Gabriel Nderumaki na wafanyakazi wa idara mbalimbali waliungana uwanjani hapo kumpa pole Mruma kutokana na msiba uliomkuta.

Wengine waliojitokeza kuupokea mwili huo uliowasili kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ), ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ‘Mwananchi Communications’ Tiddo Muhando. Msiba huo uko nyumbani kwa Mruma katika eneo la Mbezi Beach karibu na ghorofa za Benki Kuu.

Mwili wa Jerry ambaye alikuwa akisoma Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Biashara (MBA), ulipatikana mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kijana huyo kuripotiwa wakati akitoka katika hafla ya Usiku wa Mtanzania.

Taarifa ya awali iliyotolewa na chuo hicho kuhusu kutoweka kwa Jerry tangu Jumamosi iliyopita, ilisema alikuwa akitafutwa, kabla ya mwili wake kukutwa baada ya msako ulioongozwa na Kaimu Mkuu wa Usalama wa Chuo, Polisi na wanajumuiya wa chuo hicho.

-----Habari Leo

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname