Polisi wakiwa nje ya moja kati ya majengo yanayohisiwa kutumika kama
makazi ya mke na mume waliokamatwa Alhamisi kwa tuhuma za kujihusisha na
utumwa. Mmoja kati ya watuhumiwa hao ametokea Tanzania. PICHA | LEON
NEAL-AFP
Kamanda wa polisi wa London Steve Roadhouse amesema watuhumiwa hao,
ambao ni mke na mume wenye umri wa miaka 67, ni wahamiaji waliokwenda
London kwenye miaka ya 1960 kutoka India na Tanzania.
Polisi wanahisi watuhumiwa hao walikutanishwa na wanawake hao watatu
katika “harakati za kisiasa” zilizopelekea waanze kuishi “kijamaa”
kwenye nyumba moja.
Haijulikani hali ilibadilika vipi, lakini inaelekea kwenye miaka ya
1980, kibao kilibadilika, na wanawake hao watatu wakajikuta wakigeuzwa
vitwana wa timu hiyo ya mke na mume.
“Tumeanza kuwachunguza wahusika wote katika kikundi hiki cha kijamaa,”
Kamanda Roadhouse alisema mapema Jumamosi na kuongeza, “Tunatazama jinsi
walivyofanya kazi.”
Kesi hiyo ya utumwa ambayo imezigusa nyoyo za mamilioni dunia nzima
ilianza kurindima Oktoba 25 baada ya mmoja kati ya watumwa hao kupiga
simu kituo cha wahisani akiomba msaada, jambo lililopelekea polisi
kuanzisha uchunguzi uliofanikisha kuokolewa kwao.
Wanawake hao walioishi katika mazingira ya utwana wa kutisha kwa miongo
mitatu, ambao majina yao hayajawekwa wazi, wanatokea Malaysia, Ireland
na Uingereza. Taarifa ya polisi inasema umri wa watumwa hao ni miaka 67,
57 na mdogo kabisa ni mwanamama wa miaka 30.
Mke na mume waliokamatwa Alhamisi katika sakata hili la utumwa
walishawahi kunaswa katika mtego wa polisi kwenye miaka ya 1970, ingawa
polisi hawakuweka wazi walitenda kosa gani.
Vilevile, wanahisiwa kuhusika katika kile polisi walichokiita “makosa ya
uhamiaji,” na katika kutoa “huduma za kazi za shurti.” Wote wameachiwa
kwa masharti hadi Januari 2014 huku uchunguzi ukiendelea.
Chanzo Gazeti Mwananchi
No comments:
Post a Comment