WANAWAKE wakiwapenda wanaume hubaki na
mateso mioyoni mwao. Hii ni kwa sababu ni vigumu kumtokea mwanaume moja
kwa moja kumwaga sera kuwa unataka ‘akung’oe’.
Ni kweli kwamba, hata kama mwanaume
akimkubali mwanamke awe mpenzi wake baada ya kutokewa, imani yake huwa
hafifu kuhusu penzi la kweli la mwanamke huyo. Anaweza kumtumia kwa siku
kadhaa kisha akamwacha. Huo ndiyo ukweli.
Wanawake waliowahi kuwatokea wanaume
wanaweza kuwa na ushahidi mzuri zaidi juu ya hilo. Pamoja na hayo yote,
bado mwanamke anabaki kuwa binadamu, mwenye hisia za upendo na kutamani
baadhi ya vitu.
Anaweza kumpenda mwanaume na ni haki
yake ya msingi kabisa. Kuwa katika uhusiano na mtu unayempenda kwa dhati
ni jambo zuri. Moyo huridhia na kuwa huru katika uhusiano huo.
Hapa katika Let’s Talk About Love
tunakupa dondoo zitakazokusaidia kumsogeza mwanaume ambaye ameuteka moyo
wako na hatimaye kuwa wako moja kwa moja. Katika vipengele
vilivyotangulia nilieleza kuwa, kwanza mwanamke ni vyema ajitunze na
aweke mwonekano wake wenye kuvutia muda wote halafu pia nikaeleza kuhusu
kumvutia mwanaume kwa mambo mbalimbali hasa mavazi na mambo
anayopendelea. Sasa tunaweza kuendelea.
ASIWE KWENYE UHUSIANO
Jambo lingine la kuzingatia kwa mwanaume
huyo wakati wa harakati za kumweka mikononi mwako ni kuhakikisha hayupo
kwenye uhusiano na mtu mwingine. Kuna baadhi ya wanawake wapo tayari
kuwa na mwanaume hata kama yupo na mpenzi mwingine; hilo ni kosa na
naweza kusema ni umasikini wa kufikiri.
Kama kweli umempenda, itakuwa na maana kama utaweka makazi ya moyo wako kwake milele na siyo kwa muda mfupi tu.
JISOGEZE ZAIDI
Tayari umeshakuwa na uhakika kuwa hana
mtu, sasa unatakiwa kujisogeza karibu yake. Jizoeshe kumsalimia mara kwa
mara na kumsifia kuwa amependeza.
Kamwe usioneshe dalili kwamba wewe ni
‘maharage ya Mbeya’, ishia kwenye kujisogeza karibu yake kwa kumsifia na
kufanya mambo mengine yanayofanana na hayo na siyo zaidi ya hapo.
JENGA URAFIKI
Ukaribu wenu sasa unaweza kuwafanya
marafiki wa karibu. Kama uko naye ofisi moja au mnaishi mtaa/nyumba moja
ni rahisi zaidi. Kuwa rafiki yake wa kweli mwenye kujadiliana naye
mambo ya msingi.
Katika urafiki wenu, kamwe usiwe
mzungumzaji sana (hasa wa mambo yasiyofaa), aidha usipende kukaa naye
katika mazingira yenye vificho ambayo yataweza kusababisha kuingia
kwenye mtego mbaya.
ZUNGUMZIA ZAIDI MAISHA
Kuzungumzia zaidi maisha na kumshauri
juu ya mambo muhimu ya maisha, kutamfanya akuone wewe ni mwanamke makini
mwenye malengo mazuri katika maisha yako. Wanaume wanapenda sana
wanawake ambao vichwa vyao vinafanya kazi sawasawa.
Hii inaweza kuwa sababu itakayomfanya atamani kuwa karibu yako zaidi, jambo ambalo ndiyo shabaha ya moyo wako.
HAKUNA YEYE BILA WEWE
Kwa sababu tayari ni marafiki na
mnashirikiana baadhi ya mambo, tengeneza mazingira ya kuwa naye karibu
zaidi. Mshirikishe kwenye mambo yako, mfanye ajione si mkamilifu bila
kuwa na wewe karibu.
Hili litawezekana kwa kuishika siku
yake, kumtakia siku njema na kumjulia hali yake kazini na maendeleo yake
kwa ujumla. Kwa kuwa ni marafiki, kwa ndani lazima hisia za mapenzi
zitaibuka juu yako na utamuweka kwenye nafasi ya kufikiri kuanzisha
uhusiano na wewe.
NI WAKO TU!
Ukipitia hatua zote, bila shaka mwanaume
huyo ni wako tu. Ikiwa pamoja na vyote hivyo bado haonyeshi dalili au
hajafunguka kuwa unamhitaji, basi mwache, siyo riziki yako. Kwa nini
ung’ang’anie usipopendwa? Mada imeisha.
No comments:
Post a Comment