11 November 2013

HUYU NDO MZEE ANAEISHI KWA KUFANYA KAZI YA KUOSHA MAITI KWA MIAKA 30


Selemani Uliza akionyesha kitanda anachokitumia kuoshea maiti. PICHA | FLORENCE MAJANI 
Naingia katika lango kuu la chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Watu wengi wamesimama katika makundi, baadhi yao wakiwa na sura zilizojaa simanzi.
Hawa wanasubiri kuchukua au kuaga miili ya marehemu waliolala katika chumba hiki. Mlango wa kwanza wa chumba hiki ni mapokezi, hapa kuna vurugu za hapa na pale  kwa kuwa ndipo watu wanapopata stakabadhi za kutunzia miili ya ndugu zao.
Wengine wamekuja kuwatafuta jamaa zao waliopotea na baadhi wamekuja kuchukua miili iliyopo.
Mlango wa pili yapo majeneza matatu  ambayo tayari yana miili ya marehemu ndani, hawa wameshasafishwa, kupambwa tayari kwa kusafirishwa, kuagwa kisha kwenda kuzikwa.
 Kushoto kuna njia ndogo  inayoelekea yalipo majokofu ya rangi ya fedha. Simanzi imetawala katika eneo hilo lenye harufu ya mauti, kwani humu ndimo ilimolala miili ya marehemu, ambao wanaweza kuwa ni ndugu, jamaa na marafiki zetu. 
Katika njia hii kushoto, kuna chumba, humu wapo wanaume watatu wanamsafisha maiti mwenye jinsi ya kiume.
Amelala katika sinki, mpira wa maji ukimimina maji juu yake, huku mikono ya mmoja wa wanaume, ikimsafisha kwa ustadi mkubwa.
 Katika moja ya dirisha, kuna kitu mfano wa kabati ambacho kimejaa vipodozi vya kila aina, kuanzia wanja, rangi ya mdomo, mafuta, manukato, mkasi, viwembe na sabuni.
Mmoja kati ya watu wanaofanya kazi hii adimu ya kusafisha miili ya marehemu ni Selemani Uliza  anayesema, amesafisha miili ya marehemu kwa miaka 30 sasa.
Anasema kwa kawaida maiti inapofika huhifadhiwa katika jokofu hadi pale ndugu watakapofika na kutaka huduma nyingine zaidi ya kuhifadhi.
“Ndugu huja kumtambua marehemu wao,  wakitaka kusafishiwa, basi sisi hufanya kazi hiyo kwa moyo mweupe tena na kwa ari kuu ya kazi,” anaeleza.
Anasema kiutaratibu,  Hospitali ya Taifa ya Muhimbili hawalazimishi ndugu kuwatumia wahudumu wa chumba cha maiti kusafisha miili hiyo, bali iwapo ndugu watahitaji kupata huduma hiyo, basi watalipia na marehemu atasafishwa.
Gogo Mzome, Mkuu wa kitengo hiki cha kuhifadhi miili anasema bei iliyowekwa na Hospitali ya Muhimbili kusafisha miili ya marehemu ni Sh40,000 kwa maiti moja.
Wanavyofanya kazi
Uliza anasema  wakati wa kusafisha miili hiyo kwanza maiti hutolewa katika jokofu, baada ya hapo huwekwa katika sinki maalumu ambalo lina bomba na mpira mwembamba wa kupitisha maji.
Maiti ikishawekwa vyema katika sinki, bomba la maji hufunguliwa na kwa kutumia mpira, maiti huanza kuogeshwa na kusuguliwa kwa sabuni na brashi laini.
“Tunamsafisha kama binadamu yeyote yule anavyotakiwa kusafishwa, tunamsugua na kuhakikisha amekuwa safi. Wakati mwingine tunatumia brashi zenye uwezo wa kutoa uchafu vyema,” anasema.
Baada ya hapo,  anasema maiti hufutwa vyema kwa shuka kisha  taratibu nyingine huendelea iwapo ndugu watahitaji msaada wa aina yeyote kuhusu ndugu yao.
Kwa mfano, iwapo ndugu hawawezi kumvalisha marehemu, Uliza na wenzake humvalisha nguo ambazo zimeletwa kwa ajili ya safari yake hiyo ya mwisho.
Vilevile, iwapo  ndugu watahitaji marehemu wao apambwe, basi Uliza huifanya kazi hiyo ambapo kwa kipindi hicho, chumba hiki hugeuka kuwa saluni ya muda.
“Tunampamba marehemu kwa kutumia kila kifaa ambacho ndugu watahitaji, kwa mfano poda, kama ni mwanamke lipstiki, wanja na manukato. Kama ni mwanaume basi tunamvalisha na kumpaka mafuta,” anasema.
 Anaongeza kuwa: “Kama ndugu watahitaji marehemu avalishwe kito cha dhahabu, huwaita waje kuthibitisha kuwa ndugu yao amevalishwa kito hicho. Unajua siku hizi binadamu hatuaminiki.”
 Baadhi ya ndugu huamua kuleta vito vya thamani vya ndugu zao kama saa, pete, au mavazi yao waliyovaa katika harusi  ili kuwaenzi au kuwaonyesha upendo wa mwisho.
Uliza anasema mbali ya wanawake na wanaume pia husafisha miili ya watoto wachanga. “Naona kawaida tu ninaposafisha miili hii kwa sababu najua huyu ni ndugu yangu, na ninapomsafisha, simchukulii kuwa ni mwanamke, bali marehemu tu wa kawaida,” anasema.
 Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname