01 October 2013

Kocha Yanga amnyima mchezaji maji ya Sh500


 
 
NAHODHA wa Ruvu Shooting, Pius Aidan amelaani kitendo cha kunyimwa maji na Kocha wa Yanga, Mholanzi Ernest Brandts na kudai kuwa ni unyama na si uungwana kwenye soka.
Hali hiyo ilijitokeza Jumamosi iliyopita kwenye mchezo kati ya Yanga na Ruvu Shooting uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na Yanga kushinda 1-0.
Mara nyingi maji ambayo hutumiwa na wachezaji uwanjani ni ya chupa ndogo ambayo thamani yake haizidi Sh500 kwa chupa.
Tukio hilo lilitokea dakika ya 87 ya mchezo baada ya Cosmas Lewis kuchezewa rafu na beki wa Yanga, Kelvin Yondani kwenye eneo la Yanga na kuanza kuuguzwa ndani ya uwanja.
Wachezaji wa Ruvu na wale wa Yanga walikwenda kwenye benchi la Yanga na kuomba maji kukata kiu ndipo Mwanaspoti ilipomshuhudia kocha wa makipa wa Yanga, Razack Siwa akitoa maji kwa wachezaji wake Mrisho Ngassa na Haruna Niyonzima na kuwapa pia wachezaji wa Ruvu Shooting, Elias Maguni na Said Dilunga lakini Aidan alipoomba, Brandts alionyesha ishara ya kukataa naye (Aidan) akaondoka huku akitikisa kichwa.
Mchezaji huyo alisema: “Saa nyingine kocha anatakiwa kuelewa kuwa wachezaji wote ni kitu kimoja, wote tunacheza soka, kuninyima maji mimi haikuwa busara licha ya hivyo aliniambia kuwa hawezi kunipa kwa sababu nilimchezea vibaya Niyonzima kipindi cha kwanza.”
“Aliniambia kuwa nikachukue kwenye benchi letu kwani yale ni ya wachezaji wake tu, kwa kweli sikufurahishwa, ni kitendo cha kinyama na kisichokuwa na utu kumnyima binadamu mwenzio maji,” alisema beki huyo lakini Brandts alipofuatwa na Mwanaspoti kuzungumza alijibu kwa kifupi;  “Siwezi kuzungumzia suala hilo, ni la kawaida.”

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname