Waswahili husema, ‘nyumba ni choo’, wakiwa na maana kuwa nyumba haiwezi kuwa kamili bila kuwa na huduma hiyo ya choo.
Hata hivyo, pamoja na umuhimu wa choo,
lakini si kila nyumba iliyo na choo au hata zile ambazo zina huduma
hiyo, basi vyoo ni vibovu, havina hadhi. Zipo aina mbalimbali za vyoo
kwa matumizi ya binadamu katika maisha yake ya kawaida.
Vyoo vina matumizi mengi ingawa bado
watu wengi hasa katika nchi maskini na zinazoendelea ikiwamo Tanzania
wanatumia choo cha kuchuchumaa wakati wa kujisaidia, lakini mijini na
katika nchi zilizoendelea, wao hutumia vyoo vya kukaa.
Nyumba nyingi mijini na ofisi mbalimbali
zinazojengwa hivi sasa, huwekewa vyoo vya kukaa. Hata zile za zamani
zinakarabatiwa na kubadilishwa kwa kuwekewa hivi ambavyo vinaonekana vya
‘kisasa’.
Mgunduzi wa vyoo vya aina hii, Thomas
Crapper anasema kwa mtazamo wake aliona kukaa wakati wa kujisaidia ni
utambulisho wa ustaarabu na maendeleo.
Hata hivyo, madaktari wanapingana naye
wakisema kujisaidia katika vyoo vya kukaa kuna madhara kiafya kwa kuwa
mkao huo unaweza kuleta matokeo mbalimbali ndani ya mwili.
Utafiti uliofanywa na mtandao wa
‘naturesplatform’ umegundua kuwa matumizi ya choo cha kukaa huweza
kusababisha matatizo mbalimbali ikiwemo kansa ya utumbo mkubwa.
Mtaalamu wetu wa afya wa gazeti la
MWANANCHI, Samwel Shita anasema, madhara ya vyoo vya kukaa ni makubwa
kwani wakati mwingine yanaweza kuwa chanzo cha saratani ya utumbo mkubwa
kutokana na haja kubwa kubaki kwa muda mrefu katika utumbo huo.
Shita anasema mtu anapojisaidia haja
kubwa katika choo cha kuchuchumaa, kinasaidia haja yote kutoka kwa
sababu ya msukumo unaosababishwa na mkao huo.
“Unapokaa unakuwa umekaa katika choo
mwili unakuwa umelegea, hivyo inabidi utumie nguvu kubwa kujikamua kutoa
haja, tofauti na unapochuchumaa,” anasema Shita na kuongeza:
“Matatizo huanza hapo, unapojisaidia
ukiwa umekaa na kulazimisha kujikamua unaweza kusababisha vimishipa
vidogo katika utumbo mpana sehemu ya haja kubwa ya ndani na ya nje
kuvimba na maumivu makali husababishwa na ugonjwa unaojulikana kama
‘hemorrhoid,” anasema.
Anasema ‘hemorrhoid’ ni ugonjwa ambao
pia huitwa bawasiri. Mgonjwa hupata uvimbe katika njia ya haja kubwa na
hivyo kupata maumivu wakati wa kujisaidia na haja yake mara nyingine
huambatana na damu.
Aidha, anasema vyoo hivi pia vinaweza
kuwa chanzo cha magonjwa yanayotokana na shambukizi katika utumbo mpana,
kitaalamu ‘Inflammatory Bowel Disease’.
“Kila binadamu anapaswa kujisaidia na
kuhakikisha haja yote imetoka na kwisha kabisa, inapobakia inaweza
kusababisha maambukizi katika utumbo mpana kwa kuwa ule ni uchafu wenye
mchanganyiko wa vitu vingi,” anasema Shita.
“Haja kubwa inapokuwa tayari
imeshajitengeneza inapaswa kutoka yote, kama itabaki kipindi kirefu
inaweza pia kuleta uambukizi katika utumbo mkubwa na hata katika kidole
tumbo,” anasema Shita.
“Uchafu huu si tu unaweza kusababisha
maambukizi, lakini pia unaweza kuwa chanzo cha saratani ya utumbo
mkubwa. Wote tunajua kuwa mkusanyiko wa sumu mbalimbali mwilini
unakuweka katika hatari ya kupata saratani, hivyo tatizo hili
lisipotafutiwa ufumbuzi mapema linaweza kufikia huku,” anasema Shita.
Daktari Berko Sikirov kutoka Misri
ambaye alifanyia utafiti matumizi ya vyoo vya kukaa anasema kuwa iwapo
mtu ana tatizo la vivimbe vya ‘hemorrhoid’ linaweza kumalizika iwapo
ataacha kutumia vyoo vya kukaa.
Hata hivyo, anasisitiza kuwa tatizo hili
linaweza kwisha kama litakuwa katika hatua za awali. Kwa wenye tatizo
lililokomaa watalazimika kufuata matibabu kulingana na ukubwa wake.
Dk Sikirov anaongeza kuwa mbali na kupata vivimbe, pia mgonjwa anaweza kupata tatizo la kutokupata choo kwa muda mrefu.
Anabainisha kuwa kitendo cha haja kutoka
kidogo na nyingine kubakia husababisha kuganda katika ukuta wa utumbo
na zoezi hilo huendelea mpaka kuwa tatizo sugu.
“Haja kubwa huganda katika kuta za
utumbo, hali hii huifanya haja izunguke kwa muda mrefu na ndiyo tatizo
hili huanzia hapa,” anasema na kuongeza:
“Unapojisaidia ukiwa umekaa, ile njia ya
haja kubwa huwa kama imejifunga, inabidi utumie nguvu nyingi sasa ukiwa
na tatizo hili la kukosa haja kubwa huifanya itoke kwa uchache zaidi,”
anasema Dk Sikirov.
Aidha, anasema kupata haja kubwa mara
kwa mara ni muhimu kwa kuwa usipoitoa maana yake inazungusha sumu katika
damu jambo ambalo ni hatari kwa afya.
Anaongeza kuwa kutopata haja kubwa ni
kichocheo chenye uwezo mkubwa wa kusababisha saratani ya utumbo mkubwa
na uambukizi katika kidole tumbo.
Tafsiri ya kitabibu inasema hali ya
kukosa haja kubwa ni pale mtu anaposhindwa kuipata angalau mara tatu kwa
wiki. Hata hivyo, ili ujue afya yako ni njema unapaswa kuwa unapata
haja kubwa angalau mara moja kila siku.
Daktari Denis Burkitt aliwahi kuandika
kitabu cha maelekezo ya chakula ili kuepuka ugonjwa wa saratani. Katika
kitabu hicho alieleza namna ambavyo watu wanaweza kujikinga na saratani
za aina mbalimbali.
Akizungumzia saratani ya utumbo mpana
pamoja na kuelezea vyakula na aina ya maisha, pia aliwaasa watu kutumia
choo cha kukaa ili kujiepusha na tatizo hilo.
Anaeleza kuwa kwa Marekani pekee, watu zaidi ya 150,000 hufa kila mwaka kutokana na ugonjwa wa saratani ya utumbo mkubwa.
Mtaalamu wa Ngozi katika Chuo Kikuu cha
Sayansi ya Afya na Tiba Muhimbili (MUHAS), Profesa Kisali Pallangyo
anasema matumizi ya vyoo hivyo yanaweza kuwa chanzo cha maambukizi ya
magonjwa ya ngozi. Profesa Pallangyo anasema ni rahisi kuambukizwa
magonjwa ya ngono na ngozi kwa urahisi pale unapotumia vyoo vya kukaa
tofauti na vile vya kuchuchumaa.
Aidha, anayataja magonjwa yanayoweza
kuwambukizwa kwa kutumia vyoo vya kukaa kuwa ni kaswende, harara, mba,
kisonono, upele na mengine.
“Mtu mwenye magonjwa ya ngozi au ya
ngono, anaweza kuyaacha katika ‘sink’ anapolikalia, hivyo ni rahisi kwa
mtu mwingine ‘kuyachukua’ mara atakapokaa wakati wa kujisaidia,” anasema
Prof Pallangyo.
Anasema vyoo hivi ni hatari kwa afya
hasa pale vinapotumika katika jumuiya na kuongeza kuwa ni bora kutumia
vile vya kukaa ili kujikinga na magonjwa.
Source: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment