Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa
vyama vya siasa vya CCM, Chadema, CUF, NCCR- Mageuzi, TLP na UDP
wamekubaliana mambo mawili makubwa baada ya kuweka pembeni tofauti za
kiitikadi na kutanguliza masilahi ya taifa walipokutana jana Ikulu
jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo uliitishwa na Rais
Kikwete ili kuondoa sintofahamu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliopitishwa Septemba na Bunge
lilipokutana mjini Dodoma.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya
Mawasiliano Ikulu jana jioni ilisema katika mkutano huo ilikubaliwa
kwamba vyama vyote vya siasa nchini vyenye mawazo, maoni na mapendekezo
ya kuboresha Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba
viwasilishe mapendekezo yao haraka serikalini ili ifatutwe namna ya
kuyashirikisha mapendekezo hayo katika marekebisho ya sheria hiyo.
Pia Rais na vyama hivyo walikubaliana
kwamba vyama vya siasa nchini, kama wadau muhimu katika mchakato wa
Katiba Mpya, viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano
na maridhiano kwa lengo la kusukuma mbele mchakato huo kwa masilahi
mapana ya nchi yao na mustakabali wa taifa.
“Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD)
kimepewa jukumu la kuratibu jambo hilo ikiwa ni pamoja na kuandaa
mkutano wa vyama hivyo na wadau wengine nchini,” iliongeza taarifa hiyo.
Viongozi wa vyama vyama vya siasa
waliohudhuria mkutano huo ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba,
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi,
James Mbatia.
Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa CCM,
Philip Mangula, Isaack Cheyo ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa UDP,
John Cheyo na Nancy Mrikaria ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa TLP,
Augustine Mrema. Cheyo na Mrema wako nje ya nchi.
Wengine ambao waliambatana na
wenyeviti wao ni Mohamed Mnyaa na Julius Mtatiro wa CUF, Tundu Lissu na
John Mnyika wa Chadema na Martin Mng’ongo wa NCCR-Mageuzi.
Vicheko Ikulu
Vicheko na bashasha vyatawala Ikulu
Ilikuwa fursa kwa Rais Kikwete
kukutana na viongozi hao baada ya kipindi cha miezi miwili cha
kurushiana maneno baina ya viongozi wa Bunge, Serikali, CCM waliokuwa
wakivutana na viongozi wa vyama vitatu vya Chadema, CUF na NCCR-
Mageuzi.
Kama mtu yeyote angeulizwa kutabiri
katika tukio lililotokea jana lingetokea basi angekuwa na wakati mgumu
kutokana na ukali wa maneno na malumbano katika kipindi chote baada ya
kumalizika kwa mkutano wa Bunge wa Septemba.
Rais Kikwete alionekana mwenye furaha
tele wakati alipokutana na viongozi wa vyama hivyo na kivutio zaidi
ilikuwa pale alipokutana na Mnadhimu Mkuu wa Kambi rasmi ya Upinzani,
Tundu Lissu.
Viongozi hao walisalimiana huku wote
wakitabasamu na kuashiria kuwa waliamua kuweka tofauti zao pembeni na
kuangalia masilahi ya nchi.
Kumbuka katika hotuba yake ya mwisho
wa mwezi Septemba, Rais Kikwete alimshutumu Lissu kwa kusema kwamba
katika uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa yeye
hakuheshimu mawazo ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na
Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).
Rais Kikwete alikaririwa akisema
kauli hiyo ya Lissu ni uzushi, uongo na uzandiki wa hali ya juu, huku
akisisitiza kuwa mbunge huyo alitoa kauli hiyo ili kupotosha ukweli na
pengine isaidie kujenga hoja yake ya kutaka Rais asiteue wajumbe 166 wa
Bunge Maalum la Katiba.
Lissu, ambaye pia ni Mbunge wa
Singida Mashariki, alipinga tuhuma hizo na kusisitiza Rais aliteua
wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoka Baraza la Maaskofu
Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) bila ya ridhaa yao.
Chikawe, Wassira na Lukuvi ndani
Mawaziri watatu, ambao walitetea kwa nguvu kupitishwa kwa muswada ule ndani na nje ya Bunge walihudhuria mazungumzo hayo.
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, Waziri wa
Sheria na Katiba, Mathias Chikawe na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya
Rais anayeshughulikia Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira walikuwemo
kwenye mazungumzo ya jana.
Mawaziri hawa kwa nyakati tofauti
walitetea kuwa mchakato wa muswada ule haukuwa na matatizo yeyote na
kushikilia kuwa lazima Rais lazima asaini muswada kwani ulikuwa
umepitishwa kihalali na Bunge.
Pia walikuwa wameshikilia kuwa safari hii kulikuwa hakuna mambo ya mazungumzo kati ya Rais na upinzani.
Chanzo cha sintofahamu
Wabunge wa vyama vya Chadema, CUF na
NCCR-Mageuzi walisusia mjadala wa muswada huo wakipinga matayarisho yake
kutoshirikisha upande wa Zanzibar na pia walikuwa hawakubaliani na
baadhi ya vipengele vya muswada huo.
Katika hatua nyingine, taarifa kutoka
Ikulu zilisema kwamba Rais Kikwete alisaini muswada huo tangu Oktoba 10
mwaka huu siku ambayo wapinzani walipanga kufanya maandamano nchi
nzima.
Katika mahojiano na Mwananchi jana
jioni, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema muswada
huo tayari ulikwishasainiwa na Rais na kama kuna marekebisho yatafanywa.
Mwananchi ilimtafuta Rweyemamu baada
ya kusikia akithibitisha kusainiwa kwa muswada huo katika mahojiano na
BBC Idhaa ya Kiswahili jana.
Akizungumza na Mwananchi Rweyemamu
alisema, “Rais ameshasaini tangu Oktoba 10, unajua kulikuwa hakuna
tatizo lolote kuhusu muswada huu kwa sababu ulifuata taratibu zote
bungeni.”
Rweyemamu alisema kuwa awali Ikulu ilitoa taarifa kuwa Rais atakutana na wapinzani, pia atausaini muswada huo.
“Muswada umepitishwa bungeni na yeye
amekamilisha kazi kwa kuusaini ili kuwa sheria. Alipokutana na wapinzani
leo (jana) amewaeleza hilo na wameridhika” alisema Rweyemamu.
No comments:
Post a Comment