BILA STEPS INAWEZEKANA
Kwa
muda mrefu nimekuwa nikiulizwa sababu ya kuamua kusambaza filamu zangu
mwenyewe badala ya kuzipeleka kwa wasambazaji ambao nilikuwa nikifanya
nao kazi kwa muda mrefu, yaani kampuni ya Steps Entertainment.
Najua
maswali yamekuwa mengi kwa kuwa kuna watayarishaji wengi wa filamu
nchini wanaohangaika usiku na mchana ili kupata mkataba wa kufanya kazi
chini ya kampuni hiyo kwa kuwa Steps Entertainment ndiyo kampuni ya
usambazaji inayolipa vizuri zaidi kuliko makampuni mengine yote kwa
sasa.
Leo nimeamua kuongea walau kidogo …….
“Kwanza
nikiri kuwa maneno ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania,
mhesimiwa Dr. Jakaya Kikwete aliyotamka siku aliyoiita Ikulu kamati ya
mazishi ya marehemu Steven Kanumba ndiyo yamekuwa yakinisukuma sana hadi
kufikia uamuzi huu mzito.
Kati
ya waliounda kamati hiyo iliyoitwa Ikulu, mimi nilikuwa katibu,
Mwenyekiti alikuwa Gabriel Mtitu au maarufu kama Mtitu Game, pia
kulikuwa na wajumbe wengine kama Ruge Mutahaba, Asha Baraka, Jacob
Steven ‘JB’ na Mzee Chilo. Baada ya kuongea mengi kuhusiana na msiba wa
Kanumba na mazishi yake, mheshimiwa rais aliuliza ‘Hivi marehemu Kanumba
kaacha filamu ngapi?”
Kwa
aibu tulimjibu mheshimiwa rais kuwa marehemu Kanumba hajaacha hata
filamu moja, zote ni za msambazaji wake na hata mbili ambazo zilikuwa
hazijatoka yaani ‘Ndoa yangu’ na ‘Love & Power’ tayari zilikuwa ni
za msambazaji kutokana na aina ya mkataba tunayoingia na msambazaji.
Mheshimiwa
Rais alisikitika sana, akatuambia kuwa yeye hawezi kutumia nguvu
kutukataza kuuza mali zetu lakini angependa kuona kuwa tunamiliki
wenyewe filamu zetu na tutakapoona tumekwama tumwambie. Aliongeza kuwa
kuuza haki zetu ni kama kuuza utu wetu. Maneno ya mheshimiwa Rais
yalinichoma sana.
Mimi
ni msanii wa kwanza kufanya kazi na kampuni hiyo kama mtayarishaji wa
filamu na filamu yao ya kwanza kuisambaza ilikuwa ni ‘Jeraha la Ndoa’
ambayo niliitengeneza mimi. Na kwa kuthibitisha hilo, mwaka huu kampuni
hiyo ya Steps ilitoa tuzo ya heshima kwa kampuni yangu ya 5 Effects
Movies Ltd kwa ajili hiyo.
Nasikitika
kukiri kuwa filamu zote ambazo nilizitengeneza kisha zikasambazwa na
kampuni ya Steps, siyo zangu tena. Kampuni hiyo imekuwa ikinunua haki
zote za filamu wanazopelekewa kwa ajili ya kuzisambaza kwa hiyo baada tu
ya kusaini mkataba wao unakuwa huwezi kufaidika tena na chochote
kutokana na mauzo au faida nyingine zinazotokana na filamu yako.
Kwa
aina ya mikataba ambayo wasanii na watayarishaji tunaingia na kampuni
ya Steps Entertainment, sisi tumekuwa ni wasimamizi tu wafilamu za zao,
yaani ni kama manyapara kwenye mashamba ya mkonge wakati kwa ukoloni. Ni
waajiriwa tusio na mafao ya uzeeni.
Kwa
taarifa tu ni kwamba filamu zote mnazoziona mitaani zikisambazwa na
kampuni siyo za hayo makampuni yanayotajwa kutengeneza filamu hizo bali
ni filamu za Steps Entertainment. Ndiyo maana hata ukienda kwenye Chama
cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) utakuta wasanii wakubwa hawamiliki
kabisa filamu lakini kampuni ya Steps inamiliki filamu zaidi ya 400.
Kifupi
ni kuwa hadithi ni zetu, sehemu za kuigizia ni zetu, tunaigiza sisi,
tunarekodi na kuhariri sisi lakini filamu ni za Steps Entertainment na
ndiyo maana hata kampuni ya marehemu Steven Kanumba ‘Kanumba the Great’
imesambaratika baada ya kifo chake na mama yake akikabiliana na ugumu wa
maisha lakini filamu za Kanumba bado zinatesa kwenye soko la filamu
ndani na nje ya nchi.
Nawashangaa
watu wanaomshutumu mama mzazi wa Kanumba kuwa amemaliza mali za mwanae
na sasa anaishi kwa kufadhiliwa na Lulu, wangejua kilicho nyuma ya pazia
wangemuonea huruma badala ya kumshutumu. Wakati Steps wanakiri kuwa
filamu iliyowahi kuuza sana katika historia ya kampuni yao ni ‘Ndoa
yangu’ ya Kanumba, hawasemi kuwa familia yake imenufaika vipi zaidi ya
kupewa tuzo.
Pamoja
na kununua haki zote za filamu, kampuni ya Steps hawatoi malipo ya
filamu wanazozinunua kwa muda muafaka hivyo kutufanya tuendelee kuwa
mafukara siku hadi siku. Hii ni sababu ya pili ya mimi kujitoa Steps,
sitaki familia yangu ije kudhalilika baada ya kifo changu.
Fikiria
unapeleka filamu yako Steps, mnaingia mkataba wa kuuziana, lakini
hawakulipi mpaka wakati watakapoamua kuiingiza sokoni hivyo hata wakikaa
mwaka bila kuiingiza utakaa mwaka mzima unasuburi pesa. Hivi kweli
mwaka huo utakuwa unakula nini kama umeamua kuifanya sanaa kuwa kazi
yako?
Cha
kuchekesha hata wanapoamua kuiingiza sokoni hawakulipi mpaka baada ya
wiki mbili au tatu baada ya filamu yako kuwa imeingia sokoni, utasema
hapo wamekulipa au umejilipa mwenyewe baada ya kuwa imenunuliwa?
Mfano
mwingine hai ni wa marehemu Said Juma Kilowoko (Sajuki) ambaye ni
miongoni mwa wasanii maarufu na watayarishaji wa filamu. Marehemu Sajuki
alilazimika kuzunguka na wasanii wenziye mikoani akiwa anamuwa taabani
ili tu aweze kupata fedha za matibabu jambo ambalo naamini lilimzidishia
matatizo ya kiafya.
Na
kutokana na kuuza haki zetu zote ilibidi mkewe Sajuki, Wastara
atengeneze ‘Mr & Mrs Sajuki’ ili aweze kupata fedha za kujikimu na
kurekebisha mambo mbalimbali yaliyovurugika wakati akimuuguza mumewe.
Kama tungekuwa hatulazimiki kuuza haki zetu zote, familia hiyo ingeweza
japo kupeleka filamu zake kwenye vituo vya runinga barani Afrika ambako
ni chanzo kingine cha mapato kwa msanii.
Baada
ya kutafakari kwa kina niliamua kulipia leseni ya usambazaji wa filamu
kupitia kampuni yangu ya 5 Effects Movies Ltd ili niwe nasambaza filamu
zangu nikitegemewa kupata sapoti kubwa kutoka kwa wasanii wenzangu hasa
mastaa wakubwa lakini imekuwa kinyume chake. Kwa sasa naonekana adui mbele ya wenzangu.
Kupitia
kampuni yangu ya 5 Effects Movies Ltd, niliingiza sokoni filamu ya
‘Omega the Confusion’, na ndani ya masaa matano ya kwanza nilifanikiwa
kurudisha gharama zangu zote na kupata faida kidogo. Toka hapo hadi sasa
inaendelea kukimbia sokoni hivyo natengeneza faida tu na bado filamu ni
yangu, naweza kuifanyia chochote kama kuipeleka kwenye runinga za
kimataifa n.k
Nimalizie
kwa kuweka wazi kuwa sina ugomvi wowote na kampuni ya Steps, mmiliki
wake wala mtumishi yeyote wa kampuni hiyo. Pia sina chuki na yeyote kati
ya wanaoendelea kufanya kazi chini ya kampuni hiyo. Kikubwa ni kuwa
haya ni maisha na kila mmoja ana mtazamo wake katika kuyakabili na
kujiletea mafanikio”.
“WOGA WAKO NDIO UMASKINI WAKO”
‘TEAM NYATI’
No comments:
Post a Comment