19 September 2013

RIPOTI YA GAZETI LA RAIA MWEMA KUHUSU KUACHIWA HURU KWA AGNESS MASOGANGE NA MELLISA



WATANZANIA wawili, Agnes Gerald (Masogange) na mwenzake Melissa Edward waliokamatwa nchini Afrika Kusini kwa madai ya kusafirisha kilo 150 za dawa za kulevya wanayo nafasi kubwa ya kuachiwa wakati wowote kuanzia sasa, Raia Mwema limeambiwa.
 
Ingawa ripoti za awali zilieleza kwamba Watanzania hao walikuwa wamesafirisha kilo 150 za dawa aina ya Crystal Methamphetamine zenye thamani hiyo nchini Afrika Kusini wakati zikisafirishwa kutoka Tanzania, imebainika kwamba adawa walizobeba zinafahamika kwa jina la Ephedrine ambazo hazimo katika kundi la dawa za kulevya.
 
Watanzania hao walikamatwa nchini Afrika Kusini katika Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo jijini Johannesburg wakiwa na dawa hizo zilizokadiriwa kuwa na thamani ya Sh bilioni 6.8.
 
Hata hivyo, Ephedrine –dawa ambayo sasa imebainika kuwa ndiyo waliyosafirisha akina dada hao inaangukia katika kundi la vibashirifu (precursors) yaani dawa ambazo malighafi yake inaweza kutumika kutengeneza dawa za kulevya.
 
“Kusema kweli nguvu ya kesi ya akina Masogange imepungua sana mara baada ya kubainika aina ya dawa walizokuwa nazo. 

"Kama zingekuwa ni dawa za kulevya, mambo yangekuwa mengine lakini kwa haya waliyokamatwa nayo, sidhani kama kuna kesi ngumu sana. Nataraji watapewa dhamana wakati wowote kutoka sasa,” kilisema chanzo cha kuaminika cha gazeti hili ndani ya Jeshi la Polisi. 

Masogange na mwenzake wanashikiliwa nchini Afrika Kusini tangu Julai, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Sheria ya Dawa za Kulevya ibara ya 26 (1) a na b, dawa zinazotambulika kama za kulevya hapa nchini ni kama vile Cocaine, Heroin, Mandrax, Bangi, mirungi na nyingine lakini ephedrine haimo katika kundi la dawa za kulevya.
 
Ni sheria hiyo ambayo imetamka wazi kwamba mtu anayekamatwa na dawa hizo zikiwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 10 haruhusiwi kupewa dhamana lakini zikipungua thamani hiyo, anaweza kupewa dhamana.
 
Vyanzo vya Raia Mwema vimebainisha kwamba kwa vile Ephedrine si dawa za kulevya kwa mujibu wa sheria zilizopo, watuhumiwa hao wanaweza kupewa dhamana.
 
Kwa mujibu wa mwongozo wa wadau wa mapambano dhidi ya Dawa ya Kulevya uliotolewa mwaka 2011, uingizwaji na matumizi ya dawa kama hizo zinazofahamika kwa jina la vibashirifu, unatawaliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).
 
Gazeti hili lilipiga hodi katika ofisi za TFDA jijini Dar es Salaam ambako lilielezwa kwamba vibashirifu huingizwa nchini kwa utaratibu maalumu kulingana na mahitaji ya kitaifa yaliyopo.
 
“Unapozungumzia vibashirifu, unazungumzia mambo ya kitaalamu. Nitakupa mfano, kuna mmea unaitwa Coca. Mmea huu unatengeneza dawa za kulevya zinazofahamika kwa jina la cocaine lakini ni mmea huo huo ndiyo unatengeneza soda ya Cocacola ambayo karibu kila mtu anatumia.

“Mtu anaweza kutumia Ephedrine kutibu magonjwa kama vile mafua lakini anaweza kuitumia pia kama dawa za kulevya. Unajua baadhi ya dawa zilizo kwenye kundi la dawa za kulevya zinatumika pia hadi kwenye hospitali mbalimbali lakini kwa shughuli na kiwango maalumu.
 
“Mtu akitaka kuagiza dawa hizo ni lazima apate kibali kutoka kwetu. Tukizikamata kwa mtu ambaye hana kibali tunaziteketeza. 

Hiyo ndiyo adhabu ya kwanza lakini kama kutaonekana kulikuwapo na nia ya uhalifu, basi mkono wa sheria utachukua mkondo wake, alisema mmoja wa maofisa waandamizi wa TFDA aliyezungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa jina kwa kuwa si msemaji rasmi wa mamlaka hiyo.

Kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia, matumizi ya Ephedrine yalianza nchini China miaka zaidi ya 200 Kabla ya Kristo na inapatikana sana katika mmea wa Ma Huang ambao unatumika kutibu magonjwa mbalimbali katika tiba za Kichina.
 
Mwaka 1994, aliyekuwa nahodha wa timu ya soka ya taifa ya Argentina, Diego Maradona, aliondolewa kwenye mashindano ya Kombe la Dunia nchini Marekani na baadaye kufungiwa kucheza soka baada ya kukutwa na hatia ya kutumia Ephedrine ambayo ni miongoni mwa dawa zilizopigwa marufuku michezoni.
 
Raia Mwema limekosa taarifa za kwa nini vyombo vyote vya habari vya Afrika Kusini viliripoti kwamba dawa walizokutwa nazo zilikuwa ni Methamphetamine lakini sasa taarifa mpya zinataja kuwa ni Ephedrine.

Hata hivyo, nyaraka tofauti ambazo gazeti hili limezipata zinaonyesha kwamba Ephedrine na Methamphetamine zinafanana kila kitu tangu kwenye muundo wa molekyuli (chembe) zake isipokuwa Ephedrine ina kitu kinachoitwa Hydroxil ambacho hakipo kwenye Methamphetamine.

Akizungumza na gazeti hili kuhusu taarifa hizi mpya, Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa, alisema anafahamu kuhusu hilo lakini wao wanaendelea na upelelezi wao kuhusu watu waliowatuma akina dada hao kupeleka dawa hizo nchini Afrika Kusini.
 
“Haya mambo yanafanyika huko Afrika Kusini na sisi hatuwezi kuingilia labda kama wakitaka kitu kutoka kwetu. Cha msingi kwetu ni kwamba dawa hizo zilitoka kwetu na wasichana wale hawana uwezo wa kuwa na mzigo wenye thamani ile. 

Tunawatafuta wahusika na tukipata taarifa tutawapa,” alisema Nzowa ambaye anatajwa kujijengea heshima kubwa kwenye vita hii dhidi ya dawa ya kulevya

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname