INGAWA duka la Westgate liko karibu
dakika 15 tu kutoka nyumbani kwangu, nilikuwa nikienda kule kwa nadra
kununua vitu. Mara kwa mara huwa kuna watu wengi katika duka hili katika
siku za mwisho mwa wiki na hivyo niliona kama karaha. Jumamosi ilikuwa
maalumu kwa sababu nilitaka kutumia muda wangu na mkwe yangu, Amina (si
jina halisi) na baadhi ya marafiki zetu ambao watoto wao walikuwa
wakishiriki katika shindano la upishi.
Tulikuwa juu ya ghorofa la mwisho saa 5.00 asubuhi. Shindano la upishi lilikuwa likiendelea.
Baada ya muda, Amina aliamua kuelekea
chini kwa ajili ya kununua vitafunwa. Sikuwa na njaa sana hivyo niliamua
kubaki hapo hapo. Nilitaka kuangalia watoto wakipika.
Karibu saa saba na robo, Amina alikuwa
hajarejea nilipokuwa, lakini sikuwa na hofu na nilibakia hapo hadi
niliposikia sauti ya milio ya bunduki.
Nilishikwa na kihoro na kumpigia simu mwanangu. Ni ofisa usalama na nilidhani pengine angeweza kusaidia.
“Kuna milio ya risasi hapa. Naweza kusikia milio ya risasi. Tafadhari fanya unaloweza,” nilimwambia.
Niliongea naye kwa muda mfupi kwa simu
kwa sababu nilitaka kuzungumza na mkwe wangu. Katika simu aliniambia
kuwa alikuwa amejificha katika benki iliyo kwenye kituo hicho cha
biashara. Alisisitiza kwamba yu salama na alitaka niwe mwangalifu.
Mazungumzo yetu yalihitimishwa ghafla
nilipoona watu wawili wakija juu. Walikuwa na bunduki na haikunichukua
muda nikaona mabomu ya kutupwa kwa mkono yakining’inia katika mikanda
yao.
Nyuso zao hazikufichwa na tuliziona wazi
kana kwamba walikuwa hawajali iwapo tungeweza kuwatambua baadaye. Mara
moja nilianza kuwa na wasiwasi huenda nisitoke hai.
Katika kitambo hicho, hofu yangu ilikuwa
kubwa. Magaidi walipoanza kurusha risasi na magurunedi holela, umati
ukaangua kilio kwa kihoro.
Watu walianza kukimbia kwa mshtuko huku
mwelekeo wao ukiwa haueleweki. Nami nilikimbilia katika hema lililokuwa
likitumika kama jiko la watoto na kujificha humo.
Awali nilidhani walikuwa wakifyatua
risasi kwa bahati mbaya. Hata hivyo, punde nikaona kwamba wale watu
waliokuwa wakikimbia huko na huko wakipiga kelele ni wale waliokuwa
wamepigwa risasi. Huku kukiwa na makelele, niliwasikia magaidi wakiwaita
Waislamu:
“Kama ninyi ni Waislamu, mnaweza kunyanyuka na kuondoka,” walisema.
Lakini haikuwa rahisi kama
ilivyodhaniwa. Waislamu walitakiwa kuthibitisha imani yao. Walitakiwa
kutaja jambo fulani kutoka aya za Korani kabla ya kuachiwa. Na hata
baada ya hapo bado unaweza kupoteza maisha yako. Mwanamke mmoja ambaye
alisema alikuwa Muislamu lakini hakuonekana kuwa Muislamu alipigwa
risasi na kufa.
Sina uhakika kwa nini sikutumia dini yangu ili kujiokoa mapema. Pengine ilitokana na hofu. Pengine ilitokana na hali ya ukaidi.
Nikiwa nimejificha nyuma ya maboksi na
meza katika hema, watu nisiowajua wakawa wa karibu nami kuliko marafiki.
Magaidi lazima walijua tulipo; kulikuwa na maeneo mengi ambayo
tungeweza kuyatumia kujificha.
Hata hivyo, tulitulizana wenyewe kwa
wenyewe huku tukiwataka watoto wanyamaze kwa sababu sauti zingeweza
kutufichua pale tulipo.
Lakini pamoja na juhudi zetu zote za kuwatuliza wanyamaze, bado baadhi ya watoto hawa hasa wale wadogo walilia.
Tuliomba. Tuliwasilisha maombi yetu kimyakimya kwa Muumba wetu, pengine tukiona hiyo ni siku yetu ya mwisho kuwa hapa duniani.
Tulikuwa tumejificha kwa dakika 20
wakati nilipomsikia mmoja wa magaidi akipokea simu kupitia simu yake ya
mkononi. Hakuzungumza kwa sauti kubwa, lakini ilikuwa sauti tulivu ya
Kiswahili iliyosikika vema masikioni.
Maneno halisi ilikuwa vigumu kuyakumbuka. Lakini alisema kuwa ameua watu wengi na wengine zaidi walijeruhiwa.
Dakika chache baadaye baada ya kupokea
simu, magaidi walirusha risasi ovyo juu ya paa na kuondoka. Nikadhani
kwamba milio hiyo ya mwisho ililenga kutuogopesha na kutuonya tusijaribu
kuondoka mahali tulipo.
Tuliokolewa muda mfupi baadaye na wakati
nikitembea kutoka katia jengo hilo tuliona miili ikiwa imezagaa
sakafuni, nilijisikia nisiye na msaada kwamba sikuweza kufanya lolote
kuzuia hali hii.
Nilikuwa huru lakini mkwe wangu alikuwa
bado amenasa katika jengo. Nilipompigia simu alinihakikishia kuwa yu
salama tena kwa sauti tulivu. Alinitaka nisiwe na wasiwasi, ombi ambalo
halikuwezekana kwangu.
Amina aliokolewa saa 12 jioni. Saa
kadhaa nikiwa nyumbani kwa mwanangu na kwa rafiki yangu kusubiri neno la
matumaini kutoka kwake ilikuwa tete hakika.
Nilifarijika sana wakati alipompigia simu mwanangu akimtaka aende kumchukua kutoka Visa Oshwal.
Saa zaidi ya 24 baada ya ile iliyokuwa
siku njema nikiwa na mkwe wangu iligeuka kuwa jinamizi, na bado
ninatetemeka nikiikumbuka. Hata hivyo, nina furaha kuwa hai na
ninashukuru Amina na mimi tulitoka Westgate bila majeraha.
*Hii ni simulizi ya mmoja wa watu waliookoka katika tukio la ugaidi la Westgate
No comments:
Post a Comment