30 September 2013

SERIKALI YASUTWA KUHUSU KUYAFUNGIA MAGAZETI YA MWANANCHI NA MTANZANIA,YADAIWA KIKWETE KAZIDIWA NGUVU




                SIKU mbili baada ya serikali kutumia sheria ya magazeti ya mwaka 1976 inayolalamikiwa na wadau wa sekta ya habari kuyafungia magazeti mawili ya kila siku ya Mwananchi na Mtanzania, wadau mbalimbali wamejitokeza na kuipinga adhabu hiyo.
 
Sheria hiyo inampa ruhusa waziri mwenye dhamana ya habari kupiga marufuku uchapaji na matumizi ya gazeti lolote ambalo anafikiri liko kinyume na maslahi ya umma.
 
Katika adhabu hiyo, gazeti la Mtanzania limefungiwa kwa siku 90 huku Mwananchi likifungiwa kwa siku 14, adhabu mbazo zimeanza Septemba 27, mwaka huu, yakidaiwa kuchochea.
 
Wakizungumzia adhabu hizo, wadau hao, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azavel Lwaitama, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) na mwandishi nguli, Ndimara Tegambwage walidai kuwa serikali imeendelea kutumia sheria mbovu kubana uhuru wa habari nchini.
Zitto: JK amezidiwa Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Zitto alisema kuwa serikali imechukua uamuzi huo kwa kutumia sheria ya kidikteta ya magazeti ya mwaka 1976, ambayo Tume ya Jaji Francis Nyalali iliiorodhesha kama sheria kandamizi.
Alisema kuwa sababu zilizotolewa kuhalalisha uamuzi huu hazina maana, na kwamba serikali ingeweza kufungua mashitaka ya kawaida mahakamani kushitaki magazeti hayo iwapo haikupendezwa na habari walizochapisha.
“Moja ya sababu ya kufungiwa kwa gazeti la Mwananchi ni kuchapisha taarifa kuhusu mishahara ya serikali. Serikali inasema habari hii ni siri.
 
“Serikali hii hii ambayo imesaini makubaliano ya kuendesha serikali kwa uwazi (Open Government Initiative) na kumwagiwa sifa na Rais Barack Obama wa Marekani, inalifungia gazeti kwa kuandika habari za mishahara ya watumishi wa serikali,” alisema.
 
Zitto aliongeza kuwa mishahara kuanzia wa rais hadi mtendaji wa kijiji haipaswi kuwa jambo la siri.
 
“Kwamba kuonyesha kuwa jambo hili linapaswa kuwa wazi, mkutano ujao wa Bunge tutatafuta kila namna kutaja mshahara wa rais, makamu wa rais, waziri mkuu na baadhi ya watendaji wa mashirika makubwa ya umma kama njia ya kuwaunga mkono gazeti la Mwananchi kwa habari yao hiyo,” alisema.
 
Kwa mujibu wa Zitto, mapato ya mbunge yanajulikana sasa kuwa ni sh milioni 11.2 kwa mwezi kabla ya kuongeza posho za vikao za sh 200,000 kwa siku na posho ya kujikimu ya sh 130,000 kwa siku.
 
“Watanzania wana haki ya kujua wanawalipa kiasi gani watumishi wao. Tutaanza na mshahara wa rais,” alisema. Alisema kuwa gazeti la Mtanzania limefungiwa pamoja na mambo mengine kwa kuandika ‘mapinduzi ni lazima’. Kwamba inashangaza Serikali ya CCM inaogopa neno mapinduzi.
 
“Marehemu Mzee Steven Salum Nandonde, aliyekuwa mbunge wa Tandahimba alipata kusema bungeni kuwa ‘lazima nchi ipinduliwe’. Ni matumizi ya lugha tu. Mzee Nandonde yeye alikuwa analalamikia maendeleo duni ya mikoa ya kusini na kutaka kaskazini iwe kusini na kusini iwe kaskazini,” alisema.
 
Zitto aliongeza kuwa serikali inafungia gazeti kwa sababu ya kuandika ‘Mapinduzi ni lazima’ ilhali kila siku Zanzibar wanasema ‘Mapinduzi daima’.
 
“Gazeti la Mtanzania linahaririwa na Absalom Kibanda, mwandishi wa habari ambaye bado anaponya majeraha ya mwili na kisaikolojia ya kuteswa na watu ambao hadi leo hawajakamatwa.
 
“Badala ya serikali kuwakamata watesaji wa Kibanda, inamnyima kazi Kibanda ili ateseke kwa njaa kwa kukaa miezi mitatu bila kazi,” alisema.
 
Pia aliongeza kuwa inawatesa Watanzania kwa njaa ya kupata habari ambayo ni haki ya msingi ya kikatiba. Kwamba hiyo ndiyo zawadi serikali inampa Kibanda baada ya kung’olewa kucha, kunyofolewa jicho, kukatwa vidole na kuteswa kwa namna isiyoelezeka.
 
“Matukio ya hivi karibuni na namna serikali inavyoyachukulia yanaonyesha dhahiri kwamba Rais Kikwete kazidiwa nguvu na kundi la wahafidhina ndani ya chama na serikali yake.
 
“Rais ambaye alianza kwa kuhubiri uvumilivu wa hali ya juu, na hata yeye mwenyewe kupata kusema uvumilivu huu wengine wanauona kama udhaifu, lakini ameamua kujenga taifa la kutovumiliana,” alisema.
 
Kwa mujibu wa Zitto, rais alipata kulalamika hadharani kwamba kuna wenzake wanataka aongeze ukali, hivyo ni dhahiri kundi hili la wahafidhina sasa ndilo linalomwongoza Rais Kikwete.
 
“Kitu kimoja tu rais azingatie, kundi hili linaongozwa na maslahi binafsi ya kubakia kwenye utawala wakati yeye anapaswa kuacha ‘legacy’,” alisema.
 
Alisema kuwa Rais Kikwete asipokuwa makini atakuwa rais karatasi (lame duck) tu tunapoelekea mwisho wa utawala wake.
 
Kwamba uamuzi wa hovyo na wa kidikteta wa kufungia magazeti unamchora vibaya mbele ya wananchi na jamii ya kimataifa.
 
“Wananchi sasa waifanye serikali kujutia uamuzi wake wa kufungia magazeti. Nimeamua mimi binafsi kama mbunge (leo Septemba 30, 2013) kupeleka taarifa rasmi kwa Katibu wa Bunge ya kupeleka muswada bungeni wa kuifuta kabisa sheria kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976,” alisema.
 
Ndimara anena Katika andiko lake kwenye mtandao wa kijamii, mwandishi wa habari nguli, Ndimara Tegambwage alisema kufungia magazeti ni uhalifu dhidi ya haki.
 
Alisema: Serikali inaendelea kufungia vyombo vya habari. Orodha inaongezeka. Mara hii ni zamu ya Mwananchi na Mtanzania.
 
MwanaHALISI lilifungiwa miezi 15 iliyopita (mwaka mmoja na robo). Hakuna dalili za kulifungulia. ‘Redio mbao’ zinasema hata wamiliki wake wasiruhusiwe kuanzisha gazeti jingine. Limekuwa suala la binafsi.
 
Hatua ya serikali ya kufungia gazeti hilo imeathiri na inaendelea kuathiri waandishi, wake/waume zao na watoto wao; wazazi wao, ndugu waliowategemea, wauza magazeti, wenye maduka karibu na ofisi za gazeti hili, wauza matunda, mihogo, karanga, kahawa na kashata waliokuwa wakitua MwanaHALISI.
 
Wengi wameathirika hivyo kiuchumi. Sasa waandishi wamekuwa wabangaizaji kwa kuomba vibarua katika magazeti ya wengine. Wananchi wengi wameathirika kwa njia ya kukosa taarifa.
Mtu mmoja serikalini au kundi la watu; wanatumia nafasi zao kutaka kuua kwa njaa waandishi na familia zao; na kunyima wananchi taarifa muhimu zinazowawezesha kupata uelewa juu ya wanavyotawaliwa na jinsi ya kujinasua kutoka mkenge wa ghiliba, wizi na ufisadi.
 
Jana serikali iliongeza machungu kwa waandishi na wananchi na orodha yote niliyotaja hapo juu kwa amri ya kufungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania. Na serikali inajua. Hiyo siyo njia sahihi ya kutenda kazi. Serikali inaingilia kazi na majukumu ya mahakama.
 
Kwa ufupi, serikali inapuuza na kudharau mahakama. Kuna sheria ya magazeti ya mwaka 1976, katili kama ilivyo, lakini bado inatumika na watawala ndio wameiweka mbelekoni. Kwanini serikali haiitumii kwa njia ya kwenda mahakamani? Inaogopa nini? Woga wake ni upi?
 
Kuna Baraza la Habari Tanzania (MCT). Limejaa na linashirikisha wataalamu wa nyanja muhimu katika tasnia hii - waandishi wa habari na wanasheria. Lina uwezo mkubwa wa kusikiliza na kutolea uamuzi malalamiko ya mtu au taasisi yoyote. Serikali hailitumiii.
 Wahusika ndani ya serikali wanatumia ubabe wa amri kwa nia ya ‘kuua sisimizi kwa kutumia nyundo’, lakini nje ya mkondo wa sheria au ushauri wa kitaaluma ambao unaheshimika zaidi kuliko amri au mitulinga.
 
Kesho serikali itazima gazeti au chombo kingine cha habari. Itaondosha ajira za waandishi. Itafinyaza fursa za kujiendeleza katika taaluma hii. Itanyakua haki ya uhuru wa kupata taarifa na habari.
 
Itafanya kazi zake gizani na kwa hiyo bila mrejesho kutoka kwa jamii pana iliyokuwa inapata taarifa kupitia vyombo vya habari vinavyofungiwa.
 
Kufungia au hata kufuta chombo cha habari, licha ya kwamba ni kuvunja haki za binadamu; vilevile ni kuziba mifereji ya fikra ya jamii; kuongeza umasikini, kuasisi woga miongoni mwa watu, kujenga visima vya chuki na hasira dhidi ya serikali; kutaka watu waishi kwa umbeya na kurudisha jamii katika ujima.
 
Hatupendi kuamini kuwa haya yanatendwa na serikali inayojiita ya ‘kidemokrasia’ na inayojigamba kuwa na uwazi na utawala bora. Hapana! Kuna serikali ngapi - moja itende demokrasia na nyingine itende uhalifu dhidi ya haki ya uhuru wa habari? Ghiliba!
 
Tumependekeza tangu 1985. Kwamba serikali iache wananchi na waandishi wa habari waiseme wanavyoiona. Kama sivyo ilivyo, basi ipuuze. Kama ndivyo ilivyo, basi ijisahihishe.
 
Serikali ina maguvu mengi ya kutumia kuleta mabadiliko kwa maslahi ya watu; na siyo kwa kuangamiza uhuru wa kufikiri na kutoa mawazo. Inakokwenda serikali, siko!
 
Lwaitama Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Lwaitama alisema si sahihi kufungia magazeti na serikali kuanza kupangia wananchi wasome au wasisome nini.
 
“Tunaomba tuambiwe mahojiano hayo na maonyo yalifanyika chini ya uangalizi wa nani? Na yalifanyikia wapi? Hapa ninaona kuna kikundi kidogo cha watu fulani katika serikali wameamua kuanza kufungia magazeti kwa manufaa yao,” alisema.
Dk. Lwaitama aliongeza kuwa tuhuma zinapotolewa zipelekwe kwenye chombo cha uamuzi ili hukumu itolewe, kwamba haiwezekani serikali ndiyo inatoa tuhumu na kuhukumu yenyewe.
 
“Tumekuonya, hatupendezwi na uandishi wako, hivyo tunakufungia siku 14 au siku 90,” hizi ni kauli za utawala wa kibabe, na udikiteta. Hakuna dhana ya utawala bora,” alisema.
 
Alihoji kuwa kama kosa ni uchochezi, mbona kuna kesi mahakamani inayomhusu Kibanda na mwandishi Samson Mwigamba wakidaiwa kuchapisha makala ya uchochezi?
 
Kwamba kesi hiyo ina utofauti gani na tuhuma hizi zinazoitwa uchochezi hadi kusababisha magazeti ya Mwananchi na Mtanzania kufungiwa bila kupelekwa mahakamani?
 
Dk. Lwaitama alisisitiza kuwa kitendo kilichofanywa ni kama vile Tanzania hakuna mahakama wakati rais anateua majaji kila mara, na hivyo kuhoji kazi zao ni zipi kama mawaziri wanajipangia hukumu.
 
Wanaharakati Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THIRD Coalition), Onesmo Olengurumwa alisema leo wanakutana na wadau mbalimbali wa habari kwa lengo la kujadili na kutoa tamko rasmi kuhusiana na suala la kufungiwa magazeti hayo.
Alisema mara baada ya kukutana watazungumza na waandishi wa habari kutoa maazimio waliyofikia katika kikao hicho.
Hata hivyo, alisema sheria ya magazeti ya mwaka 1976 ni kandamizi na inahitaji kuondolewa.
Olengurumwa aliongeza kuwa sheria zilizopo zinakandamiza uhuru wa vyombo vya habari.
 
“Sheria hii ni kandamizi kwa kuwa serikali wao ndio walalamikaji, lakini wao wenyewe wanatoa uamuzi bila kushirikisha upande wa pili, jambo ambalo ni unyimwaji wa uhuru wa vyombo vya habari,” alisema.
 
Zanzibar wacharuka Jumuia ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (Wahamaza) nayo imeungana na watetezi wa uhuru wa vyombo vya habari kusikitikia uamuzi wa serikali kufungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania.
 
Katibu wa Wahamaza, Salma Saidi alisema uamuzi wa serikali umetolewa wakati wanatasnia ya habari wanadai uhuru zaidi wa habari, na wakati bado wanalalamikia kufungia gazeti la MwanaHALISI kwa muda usiojulikana.
 
“Wahamaza inaamini kuwa adhabu ya kuyafungia magazeti ni kubwa mno na haikusitahiki, na sababu zilizotolewa na serikali kuyafungia magazeti hayo hazitoshelezi,” alisema.
 
Alisema kuwa wanaamini kwamba njia bora ya serikali kujenga utawala bora wenye kuheshimu sheria ni kutumia mahakama katika malalamiko dhidi ya habari zinatolewa na vyombo vya habari.
 
“Wahamaza inatoa wito kwa wadau wa vyombo vya habari nchini kuendelea na harakati za kuitaka serikali kufuta sheria zote zitazotumia kukandamiza vyombo vya habari ikiwa pamoja na sheria ya kufungia magazeti,” alisema.
-Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname