TIMU ya soka ya Tanzania, Taifa Stars,
juzi ilimaliza kwa machungu kampeni ya kuwania nafasi ya kucheza fainali
za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil, baada ya
kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Gambia.
Ingawa Stars ilishakosa tiketi ya
kucheza hatua ya kumi bora tangu ilipofungwa mechi mbili mfululizo dhidi
ya Morocco na Ivory Coast, iliwafuata Gambia wakihitaji ushindi ili
kumaliza kampeni hizo wakiwa nafasi ya pili.
Wakati Stars inaondoka nchini, Kocha
wake Kim Poulsen, alisema wazi wanahitaji pointi tatu ili kushika nafasi
ya pili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya viwango vya timu katika
upangaji wa timu kampeni za kimataifa zikiwemo fainali za Kombe la
Mataifa Afrika za mwaka 2015.
Hata hivyo, Stars imeshindwa kupata
ushindi kwa vibonde hao wa kundi la C, waliomaliza na pointi nne
wakitanguliwa na vinara Ivory Coast (14) waliotinga raundi ya 10 bora,
Morocco (9) na Tanzania (6).
Kwetu Tanzania Daima tumepokea matokeo
hayo yasiyotarajiwa kwa masikitiko makubwa kiasi cha kuzua maswali mengi
juu ya nini kifanyike ili Stars iweze kuwa na uwezo halisi kisoka
badala ya kuwa na kiwango kinachopanda na kushuka kama homa ya vipindi.
Tunapaswa kujiuliza hivyo kwa kuzingatia
kuwa kama matunzo na mahitaji muhimu, wachezaji hao chini ya udhamini
wa Kampuni ya Bia Tazania (TBL), wamekuwa wakipata matunzo mazuri
pengine kuliko wakati wowote katika historia ya timu hiyo.
Tunajiuliza kama Stars inayopata matunzo
ya kiwango hiki inapata matokeo mabaya hivi, nini kifanyike ili timu
hiyo iweze kufanya vizuri kwenye kampeni mbalimbali za kimataifa kama
fainali za Kombe la Mataifa Afrika na Kombe la Dunia?
Inasikitisha kuona timu yetu ikizidi
kupotea ikifungwa mechi tatu mfululizo za kimataifa wakianza kufunga na
Morocco 2-1, Ivory Coast (4-2) kisha kufungwa 2-0 na Gambia iliyo nafasi
ya 163 kwa ubora wa soka ulimwenguni.
Kama Stars inashindwa hata mbele ya timu
dhaifu kama Gambia, tusitarajie miujiza ya kucheza fainali za Afrika
chini ya mazingira haya kama hakutakuwa na hatua madhubuti za kuleta
mabadiliko ya kusonga mbele.
Matokeo haya yanaonyesha wazi kumbe
tatizo la Stars ni zaidi ya udhamini kwa maana uwekezaji kwenye programu
za vijana mbinu ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa siri ya mafanikio ya
mchezo huo kote duniani.
Tunasema bila kufanya uwezekezaji huo
muhimu, hata udhamini wa mamilioni ambao umekuwa ukimwagwa kwa timu
hiyo, utakuwa ni sawa na kazi bure kwa sababu mafanikio ya kweli ya
mchezo huo yatabaki kuwa ndoto isiyotimia.
Uwekezaji tunaosema hapa ni kuanzia
klabu za Ligi Kuu kuwa na timu hai za vijana tofauti na ilivyo sasa
ambapo huwatafuta wa msimu pale wanapotakiwa kushiriki michuano ya Kombe
la Uhai ambayo hushindanisha vikosi vya vijana wa chini ya miaka 20.
Kama klabu zote za Ligi Kuu zitakuwa na
vikosi vya vijana na msisitizo ukiwekwa kwenye michuano mingine ya
vijana kama Copa Coca Cola, mashindano ya shule za msingi kuanzia shule
za msingi (Umitashumta) na sekondari (Umiseta) na Kombe la Taifa na
mingineyo, mageuzi yataonekana.
Tunasema umefika wakati sasa wa kuchukua
hatua stahiki ya kuondoka hapa tulipo kama kweli tunataka kuyafikia
mafanikio ya kweli ya soka tofauti na ilivyo sasa ambapo kila kukicha ni
heri ya jana, tuzinduke, tuchukue hatua kwa sababu jahazi linazidi
kuzama

No comments:
Post a Comment