Maandalizi ya kushambulia jengo la maduka la eneo la Westgate, Nairobi yalifanyika kwa miezi mingi.
Gazeti la New York Times la Marekani
lilikariri vyanzo vyake ndani ya vyombo vya usalama vya nchi hiyo jana
vilivyosema kuwa mipango na mazoezi kwa ajili ya shambulizi hilo
vilifanyika Somalia.
Magaidi kati ya 10 hadi 15 wa Al-Shabaab
walivamia kwa silaha kwenye jengo la ghorofa nne la maduka na
kusababisha vifo vya watu 67 kwa mujibu wa taarifa za Serikali ya Kenya
na majeruhi 175. Magaidi watano walipoteza maisha kwenye tukio hilo.
Kitengo cha Mambo ya Nje cha Kundi la Al-Shabaab ndicho kilichokuwa na kazi ya kupanga shambulizi hilo.
Imeelezwa kuwa watekelezaji wa tukio la
kigaidi walipitia mafunzo maalumu huko Somalia yaliyowawezesha kubaini
michoro ya jengo pamoja na mbinu za kusafirisha silaha.
Utekelezaji
Gazeti hilo lilidai kuwa uratibu wa
operesheni hiyo ulifanywa kwa uangalifu kwani wafuasi wa Al-Shabaab
waliochaguliwa ni wale ambao walikuwa wanafahamu vyema Kiingereza na
wenye uzoefu wa masuala ya kimataifa.
“Hawa jamaa pia waliandaa mchoro wa
jengo hilo. Wakaandaa mkakati wa kupenyeza silaha ambazo walikuwa
wamezileta kutoka Somalia,” kilisema chanzo cha gazeti hilo.
Gazeti la New York Times, lilisema
silaha zilizotumika kwenye uvamizi huo zilipenyezwa kupitia maeneo
yalikuwa yakilindwa na askari wa kampuni binafsi za ulinzi.
Duru za usalama za Marekani zimeeleza
kuwa kuna uwezekano mkubwa kuwa baadhi ya askari walihongwa kutokana na
kukabiliwa na ukata wa kutolipwa kwa wakati na waajiri wao.
Taarifa zinasema kuwa siku moja au mbili
kabla ya uvamizi huo, inasemekana magaidi hao walipitisha kwa siri
mikanda ya risasi kwa ajili ya kutumika kwenye bunduki zao aina ya
`Short Machine Gun’ (SMG).
Baadhi ya wafanyakazi wa jengo hilo
wanadaiwa kula njama na magaidi hao ili kufanikisha mpango wa kuingizwa
kwa silaha hizo zilizotumika kwenye ugaidi.
Taarifa zaidi zinasema kuwa mmoja wa
magaidi hao alikuwa amebeba nguo za kubadilisha ambazo angezitumia na
wenzake kwa ajili ya kutoka nje ya jengo hilo pamoja na raia wakati wa
kukimbia baada ya kufanya mauaji. Serikali ya Kenya imetoa orodha ya
washukiwa wa shambulizi hilo wanaotoka Marekani na Uingereza.
Rais Uhuru Kenyatta alisema taarifa za
kiusalama zimedokeza kuwa mashambulizi hayo yalitekelezwa na raia watatu
kutoka Marekani na mwanamke mmoja wa Uingereza.
Wizara ya Ulinzi ya Marekani imesema
imepokea taarifa za kuhusika kwa raia wake, lakini imesisitiza kuwa bado
haiwezi kudhibitisha moja kwa moja mpaka pale itakapopata uhakika kwa
njia ya vipimo vya kinasaba (DNA).
“Tunafahamu yaliyotokea Kenya, lakini
hatuwezi kuthibitisha moja kwa moja kuhusika kwa raia wa Marekani,
tunasubiri vipimo vya DNA pamoja na baadhi ya picha za kwenye mitambo ya
CCTV... lakini tendo lililofanyika nchini Kenya ni la kinyama,” alisema
ofisa mmoja wa usalama wa Marekani ambaye hakutaka jina lake kutajwa
alipohojiwa na New York Times.
Serikali ya Kenya imesema imedhibiti
eneo zima la jengo na kuwaua baadhi ya magaidi hao ingawa nchi za Ulaya
na Marekani zinaona kwamba kuna uwezekano baadhi ya wavamizi
walifanikiwa kutoroka wakati wa kurushiana risasi
No comments:
Post a Comment