Wakati wa Jeshi la Polisi la Tanzania
likisema linafuatilia taarifa za vitisho za kundi la Al-Shabaab la
Somalia za kushambulia, Mtanzania mmoja, Vedasto Nsanzugwanko ambaye
alijeruhiwa kwenye shambulio la Kenya ameelezea yaliyomkuta.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya
Jinai (DCI), Robert Manumba alisema jana kuwa wameanza kufuatilia kwa
undani taarifa zilizozagaa katika mitandao ya kijamii kwamba kundi la
Al-Shabaab linajipanga kuishambulia Tanzania na Uganda
DCI Manumba alikiri kusikia taarifa
hizo na kusema kuwa Jeshi la Polisi limeanza kufanya uchunguzi wa kina:
"Siwezi kukueleza ni uchunguzi wa aina gani tutakaofanya, hiyo ni siri
yetu."
Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la
Wananchi (JWTZ), Meja Eric Komba alisema kuwa kuna uwezekano taarifa
hizo zikapikwa na wajanja wachache kwa ajili ya kuwajengea hofu
wananchi.
"Taarifa za kwenye mitandao wakati
mwingine ni uzushi mtupu... kuna kipindi ziliwekwa taarifa za uongo
zinazohusu jeshi hili," alisema.
Alipotakiwa kutoa msimamo wa jeshi hilo iwapo taarifa hizo zitakuwa na ukweli alisema, "Jeshi tuko tayari kwa jambo lolote."
Mtanzania ajeruhiwa
Nsanzugwako ambaye ni Meneja wa
Kitengo cha Kulinda Watoto kwenye Shirika la Umoja wa Mataifa la
Maendeleo ya Watoto (Unicef), Kenya alisema kwamba akiwa katika
Hospitali ya Aga Khan, Nairobi alipigwa risasi miguu yote miwili.
Alisema alifikwa na mkasa huo baada ya
kupitia katika maduka hayo akitokea kazini ili kupata kahawa...
"Nilipofika baada ya nusu saa nilisikia milio ya risasi ndipo nikaona
purukushani zimeanza."
Nsanzugwako alisema alianza kukimbia
na wenzake huku wakijaribu kuokoa watoto waliokuwepo katika eneo hilo
ambao walikuwa katika shindano la mapishi lililoandaliwa na Radio Africa
Group.
"Watoto walianza kukimbilia ghorofa za juu zaidi na magaidi walianza kuwafuata.
"Baada ya hapo, waliendelea
kutukimbiza na nilikutana nao ana kwa ana na mmoja wa magaidi hao ambaye
alinifyatulia risasi na kunipiga miguu yote miwili," alisema.
Alieleza kwamba alijikongoja hadi
alipofanikiwa kutoka nje kwa kupitia mlango uliokuwa mbele yake na
kupokewa na polisi na kisha kuchukuliwa na Msalaba Mwekundu kwa ajili ya
huduma ya kwanza na kisha kupelekwa hospitalini kwa matibabu.
"Jioni yake nilitakiwa kusafiri kwenda Geneva, Uswisi kikazi lakini kutokana na tukio hilo nilishindwa kufanya hivyo," alisema.
Alisema amekuwa jijini Nairobi kwa miezi saba akiwa anafanya kazi Unicef.
Kaka wa majeruhi huyo, Mbunge wa
zamani Kasulu Mashariki, Daniel Nsanzugwako, alisema amekuwa
akiwasiliana na mdogo wake huyo na kwamba anaendelea vyema.
Nsanzugwako, ambaye aliwahi kuwa Naibu
Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo alisema mdogo wake alimweleza
kuwa tayari ameshafanyiwa upasuaji lakini bado hajaweza kutembea.
Taarifa iliyotolewa jana na Ofisa wa
Ubalozi waTanzania nchini Kenya, Shiyo Innocent ilithibitisha kuwapo kwa
Mtanzania mmoja ambaye amejeruhiwa kwa risasi katika miguu yake yote...
"Ubalozi unaendelea kufuatilia kama kuna Watanzania wengine waliokuwepo
kwenye tukio hilo."
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nchi
za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule alisema Serikali
inaendelea kufuatilia afya ya Mtanzania huyo.
"Ofisi yetu ya ubalozi iko karibu na
inafuatilia kila kinachoendelea. Kwa sasa nimeambiwa kuwa majeruhi
anaendelea vizuri na tuna matumaini atapata ahueni," alisema.
Chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment