20 July 2013

Okwi, Patrick Ochan waomba kurudi Simba


 
PATRICK Ochan na Emmanuel Okwi wamefanya uamuzi wa kushangaza baada ya wote wawili kuomba kurudi kuichezea Simba ya jijini Dar es Salaam.
Ochan, kiungo aliyeuzwa na Simba kwenda TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kiasi cha dola 100,000 
anataka kurudi Msimbazi haraka iwezekanavyo kwa uhamisho wa mkopo baada ya kuchoshwa na maisha ya Lubumbashi.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Ochan mwenye umri wa miaka 27, ameonyeshwa kukerwa na lundo la wachezaji mahiri na wasio mahiri ndani ya TP Mazembe ambalo limesababisha akose namba ya kudumu klabu hapo.
“Nataka kurudi Simba kwa mkopo, nimechoshwa na maisha ya Mazembe. Tajiri (Moise Katumbi) anarundika wachezaji wengi hapa na nafasi ya kucheza imekuwa ngumu. Waambie watu wa Simba nataka kurudi klabuni kwangu kwa mkopo. Mwambie Kaburu (Geofrey-aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Simba) nataka kurudi Simba,” alisema Ochan.
Ochan amekiri kwamba mara kadhaa amejaribu kuihama Mazembe ikiwemo kutaka kutimkia Afrika Kusini kuichezea timu ya Golden Arrows, lakini Katumbi ametia ngumu.
“Kuhama kwa mkopo inawezekana. Nitazungumza na viongozi huku nadhani inawezekana kabisa kwa sababu watataka nipate muda wa kucheza. Baada ya wiki mbili nitakuja Uganda. Kwa kweli nataka kurudi zangu Simba,” alisema Ochan ambaye aliuzwa pamoja na Mbwana Samata wakitokea Simba.
Katika hatua nyingine, Emmanuel Okwi naye amempigia simu mmoja ya viongozi wa Simba na kuomba arudi Msimbazi.
Okwi, ambaye yupo jijini Kampala akiwa amesusa kwenda Etoile du Sahel kwa mwezi moja sasa, ameomba kurudi Simba kwa madai kuwa amekuwa hapewi nafasi ya kucheza, lakini mbaya zaidi amekuwa halipwi mshahara na hajamaliziwa fedha zake za kusaini mkataba wa miaka mitatu.
“Ni kweli amepiga simu kuomba tumrudishe Simba, lakini tukifanya hivyo tutakosa Sh 480 milioni ambazo tunawadai Etoile,”alisema kiongozi mmoja wa Simba. Kiongozi huyo alisema kinachoweza kufanyika ni klabu hiyo ya Tunisia angalau iwalipe Sh 300 milioni halafu Okwi aje Simba kucheza kwa mkopo.
Mwanaspoti ilimtafuta Okwi kwa simu jana Ijumaa, lakini simu yake ya mkononi ilikuwa inaita bila kupokewa.
source mwanaspoti

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname