Kichwa kina gonga kama ngoma, unaona kizunguzungu, mwili hauna nguvu,
unasikia kichefuchefu, kama unataka kutapika lakini hutapiki, kwa kifupi
unajisikia hovyo kufuatia unywaji wa kupindukia ulioufanya jana! Hali
hii inaitwa HANG-OVER au uchovu.
Ingawa hatupendi kuelezwa ukweli
au kufikiria madhara ya pombe, lakini ni ukweli ulio wazi kuwa pombe ni
dawa ya kulevya. Ina dhoofisha mwili na pale mtu anapokunywa kupita
kiwango, mwili hujawa na sumu. Unapokutana na hali hiyo, mwili hujaribu
kujinasua kama vile ambavyo kitu chochote kingefanya kinapovamiwa na
kitu kigeni.
Njia bora ya kuondokana na uchovu (hangover) ni
kunywa kiasi au kuacha kabisa ulevi. Kama utashindwa kujizuia kunywa na
unataka kujiepusha na uchovu asubuhi, ni vyema ukila vitu vifuatavyo
ambavyo vinaweza kukusaidia:
1. NDIZI MBIVU
Unapozidiwa
na kilevi, kiasi kikubwa cha madini ya potasiamu hupotea, hivyo kwa
kula ndizi mbivu ambazo zinaaminika kuwa na kiwango kikubwa cha madini
hayo, kutakusaidia kupunguza makali ya hang-over. Unachotakiwa kufanya
ni kutafuta ndizi mbivu nzuri, menya na kula kwa wingi.
2. TANGAWIZI
Tangawizi
mbichi imekuwa ikitumika kwa muda mrefu kutibu magonjwa mbalimbali,
yakiwemo ya kusikia kichefuchefu na mafua. Andaa juisi ya tangawizi
mbichi na kunywa kama ilivyo, au unaweza kuandaa kwa kukata vipande kati
ya 10 hadi 12 na uchanganye na vikombe 4 vya maji. Chemsha kwa dakika
10, epua na chuja. Kisha changanya na juisi ya chungwa moja, kipande cha
limau na nusu kikombe cha asali. Kunywa mchanganyiko huo utapata nafuu
mara moja.
3. ASALI NA LIMAU
Asali na limau
ni kinywaji bora kuliko vyote katika tiba hii, ni rahisi kutengeneza na
kunywa. Kina rudisha haraka kiasi cha sukari na maji kilichopotea wakati
wa kunywa kilevi. Chemsha maji kiasi cha kikombe kimoja, changanya
limau na asali kupata ladha unayoitaka. Ni bora kutumia asali ili kupata
sukari ya asili, badala ya kutumia sukari ya kawaida. Ili kupata
ahueni, kunywa mchanganyiko huo mara kadhaa kwa siku.
4. SUPU, WALI (agrrrrrr mhh)
Mtu
anapoanza kupata nafuu kutokana na uchovu, chakula huwa kitu cha mwisho
kabisa kutamani kula, lakini pamoja na kutojisikia hamu ya kula,
unahitaji kula ili mwili upate nguvu. Unashauriwa kuanza kwa kula
vyakula vyepesi kama vile wali mweupe, supu, n.k
5. KINYWAJI MAALUM
Kunywa
pia vinywaji maalum vinavyotumiwa na wanamichezo kwa lengo la kurejesha
nguvu na madini yaliyopotea mwilini. Unaweza pia kunywa vinywaji vya
kutia nguvu mwili (energy drink) kama vile, Red Bull, Shark, Malta
Guiness, n.k
6. BARAFU
Ili kutuliza maumivu
ya kichwa, chukua vipande vya barafu, weka kwenye mfuko wa plastiki
ambao utazungurusha kwenye kitaulo na kuweka kwenye kipaji chako cha uso
kinachogonga.
7. JUISI
Juisi, hasa fresh ya
machungwa, husaidia kupandisha kiwango cha sukari kilichopotea na
husaidia kuondoa dalili za uchovu mwilini. Hata hivyo, kama tumbo lako
limechafuka sana, kunywa juisi ya epo (tufaha) badala ya machungwa
ambayo ina asidi.
8. MAJI
Mbali ya muda,
maji ni tiba bora ya uchovu. Upungufu wa maji unaotokana na kunywa kiasi
kingi cha kilevi ndiyo unaoleta kasheshe mwilini. Kunywa maji mengi
wakati wote wa mchana, siyo chini ya glasi nane kwa siku.
DONDOO MUHIMU
Ili
kujiepusha na ‘hang-over’ asubuhi baada ya kunywa kupita kiasi, kunywa
maji mengi sana kabla ya kupanda kitandani. Au kunywa taratibu, kinywaji
kimoja kila baada ya saa moja kwani huo ndiyo muda unaotumika na
kinywaji kusambaa mwilini na kutoweka.
No comments:
Post a Comment