Mojawapo ya ofisi za Kampuni ya Kanumba The Great Films illiyopo Sinza Mori.
MIPANGO endelevu inapaswa kufuatwa na kila mwanadamu, katika familia
zetu za Kiafrika mara nyingi tunaanguka katika suala la mipango mikakati
ya muda mrefu. Mwanadamu akifariki, mara nyingi wanaoachwa kuendeleza
kazi za marehemu wanaishia kusuasua na kutofikia malengo.Yapata mwaka mmoja tangu, aliyekuwa legend wa simema za Kibongo,
Steven Kanumba
‘The Great’ afariki dunia na kuiacha Kampuni yake ya
Kanumba The Great Film ikiendeleza shughuli zake za kuzalisha filamu
kama kawaida.
Kampuni aliyoiacha pale Sinza-Mori, jijini Dar ilibaki
chini ya mikono ya wafanyakazi wake wakiongozwa na mdogo wa marehemu,
Seth Bosco, mpiga picha za video, Zakayo Magulu pamoja na Mayasa Mrisho
‘Maya’ ambaye alikuwa akifanya kazi kama msimamizi wa ‘location’
(location manager) na masuala ya makeup.
Kadiri siku zilivyozidi
kusonga, umoja kati yao ulianza kupungua. Kila mmoja anaonekana
kuhangaika kivyake licha ya kwamba kampuni bado ipo. Mikakati ya jumla
ikawa haijadiliwi, kila mmoja akawa anaangalia namna ya kujikwamua
kivyake.
Mara kadhaa nimekuwa nikizungumza na baadhi ya wasanii
waliokuwa tegemezi katika kampuni hiyo, wamekuwa wakiniambia wapo bize
kufanya kazi zao binafsi nje ya Kanumba The Great Film. Hiyo inaonesha
dalili kwamba kazi za umoja zimeanza kulegalega.
Miongoni mwa bidhaa zilizokuwepo katika ofisi hiyo ni pamoja na DVD
za marehemu alizokuwa akiziuza lakini baada ya kifo chake, ofisi hiyo
imepoteza mvuto wa kibiashara na hata mpangilio kwa jumla. Hakuna mtu wa
kukemea au kuhakikisha mambo yanakwenda sawa.
Kabla Kanumba
hajapatwa na mauti, alikuwa mpiganaji. Alipambana kuhakikisha anafikia
malengo yake. Lengo lake lilikuwa ni kuhakikisha tasnia ya filamu
inafika levo za Kimataifa.
Enzi za uhai wake, Kanumba ndiye
aliyeanza kuthubutu kutoboa mianya ya kuwashirikisha wasanii wa Nigeria.
Alifanikiwa kucheza simema ya Dar 2 Lagos na filamu nyingine kadhaa kwa
kuwashirikisha wasanii mbalimbali wa nje ya Tanzania.
Kama hiyo haitoshi, mwaka 2011 marehemu alizidi kujitanua zaidi
katika soko la Nollywood kwa kumchukua mwigizaji mkubwa nchini Nigeria,
Ramsey Noah na kufanya naye filamu ya Devil King Dom ambayo kwa kiasi
kikubwa imeleta mapinduzi makubwa katika gemu.
Kuonesha anapenda
maendeleo, Kanumba hakuishia hapo kwani mwaka huohuo alipiga hatua
nyingine kubwa katika sanaa baada ya kufanikiwa kwenda New York,
Marekani na kununua vifaa vya kisasa vya kuzalishia filamu.
Mpaka
mauti yanamkuta Aprili 7, mwaka jana tayari alikuwa ameshajiwekea
misingi mizuri katika sanaa kwani alikuwa anamiliki kampuni yenye vifaa
vya kisasa pamoja na kutoa ajira ya wafanyakazi wasiopungua kumi.
Marehemu
alijiwekea mikataba na Kampuni ya Steps Entertainment kuzalisha filamu 6
kwa mwaka. Hilo alifanikiwa kwa kiasi kikubwa, tena aliweza kuigiza na
filamu nyingine za kushirikishwa mbali na zile za Steps.
Hadi kufikia
Aprili 7, mwaka huu marehemu alikuwa akitimiza mwaka mmoja kaburini.
Mdogo wake, Seth Bosco ambaye amejitoa kuendeleza kampuni hiyo,
amefanikiwa kuingiza sokoni filamu tatu tu.
Mbaya zaidi mbili kati ya hizo (Love and Power na Ndoa Yangu)
zilisharekodiwa na marehemu, wao wakazikamilisha kwa kuzifanyia
‘editing’. Yeye kama yeye alifanikiwa kuingiza filamu moja sokoni ya
Malaika.
Kwa mwendo huo utagundua spidi aliyoiacha marehemu
imepungua, filamu walizoingiza ni chache sana. Kifupi wanasuasua kama si
kupoteza muelekeo. Kwa mfumo aliokuwa akienda nao marehemu, mwaka mmoja
baada ya kifo hadi sasa, kampuni ilipaswa kuzalisha filamu sita au
zaidi.
Kuna kitu cha kujifunza katika mfumo ambao aliuacha marehemu. Walioachiwa kampuni wakiongozwa na Seth wanapaswa kujitazama upya.
Hii ni changamoto ngumu inayohitaji akili ya ziada kuweza kuvuka,
katika hali kama hiyo hakuhitaji masihara wala utani hata kidogo. Hapo
ndipo watu wanapotafutana uchawi. Wenye mamlaka ya kuiendesha kampuni
kwa namna moja au nyingine wanapaswa kuwa
wakali kidogo ili mambo
yaende.
Kujituma kwa marehemu ndiyo kulisababisha ashinde tuzo
mbalimbali za filamu zikiwemo zile za Zanzibar Film Festival (Ziff).
Ingependeza basi heshima ile aliyoiacha marehemu ikaenziwa kwa kuvuka
mipaka, ikiwezekana zaidi ya pale alipokuwa akipapigia mahesabu yeye
enzi za uhai wake.
Naamini inawezekana kama wahusika wataweka nia.
No comments:
Post a Comment