Di Matteo aliiwezesha Chelsea kuwa mshindi wa klabu bingwa barani
Ulaya, na vile vile kupata Kombe la FA msimu uliopita, na mwezi Juni,
alitia saini mkataba wa miaka miwli.
Lakini
kufuatia Chelsea kuzabwa magoli 3-0 na Juventus usiku wa Jumanne,
inaelekea timu hiyo itakuwa na kibarua kigumu sana cha kufanikiwa
kuendelea katika michuano ya klabu bingwa, na kwa hiyo wasimamizi wa
klabu wameonelea ni vyema kumtimua kutoka Stamford Bridge.
Kulingana na taarifa katika mtandao wa Chelsea, "klabu kitatoa taarifa kamili hivi karibuni kuhusiana na meneja wa timu".
Roman Abramovich, tajiri anayemiliki klabu ya
Chelsea, sasa atakuwa anamtafuta meneja wa tisa, tangu kumiliki klabu
mwaka 2003, na kwa muda mrefu, inaaminika amekuwa akizitamani sana
huduma za aliyekuwa meneja wa Barcelona ya Uhispania, Pep Guardiola.
Lakini vile vile amewasiliana na aliyekuwa kocha
wa Liverpool ya Uingereza, Rafael Benitez, na kuna uwezekano huenda
akashikilia hatamu kwa muda mfupi.
Abramovich, raia wa Urusi, tayari alikuwa amewasiliana na Benitez hata kabla ya Chelsea kushindwa nchini Italia.