13 February 2016

Mwanamke aliyewanyang'anya majambazi Bunduki agomea zawadi ya pesa za Polisi laki 5 ,Asema ni ndogo



Sophia Manguye, mkazi wa kata ya Sirari wilayani Tarime mkoani Mara,   jana alionesha kugomea shilingi 500,000 aliyopewa na jeshi la polisi kama zawadi ya kumtia moyo kwa ushujaa wake wa kupambana na majambazi na kufanikiwa kuwapokonya bunduki aina ya SMG hivi karibuni.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa kiasi hicho kilichotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Tarime/Rorya, Gemini Mushy, Bi. Manguye alieleza kuwa kiasi hicho ni kidogo kwa tukio la hatari alilolifanya linalohatarisha maisha yake. Hivyo, aliliomba jeshi hilo kumuongeza.
Alisema kuwa kiasi hicho hakiendani na hali halisi ya maisha yake kwani ana watoto kumi na hivi sasa maisha yake yako hatarini.
“Hii haiwezi kutosha hata kuwawezesha watoto wangu kuishi. Hata kuwalipia gharama za masomo shuleni. Ninaomba hata kidogo mkaniongezee hata shilingi ngapi… Hii zawadi kwakweli mimi siridhiki kusaini nayo kwa sababu hapa nilipo nilitoka kwenye kifo,” alisema Mwanamke huyo.
Hata hivyo, Jeshi la polisi mkoani humo lilieleza kiasi hicho ni zawadi tu kwa kutambua mchango wake kwa kupambana na uhalifu nchni na kwamba hiyo sio biashara.
Akiongea na waandishi wa habari baada ya kukubali kupokea na kuweka sahihi kwenye barua ya kukiri kupokea zawadi hiyo, mwanamke huyo alisema kuwa tukio hilo la kumnyang’anya jambazi silaha sio la kwanza kwake kwani mwaka 2014 alifanya tukio kama hilo baada ya kumpiga na kigoda jambazi aliyevamia katika eneo lao.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname