Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli amefanya
ziara ya kushtukiza kwa mara ya pili katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili leo na kubaini changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na wagonjwa
kuendelea kulala chini.
Akiwa katika wodi ya wazazi, Rais Magufuli
alishuhudia idadi kubwa ya wagonjwa inayozidi vitanda huku akina mama
waliokuwa katika wodi hiyo wakimueleza kuwa wanalazimika kulala zaidi ya
watatu kwenye kitanda kimoja.
Hali
hiyo imedhihirika ikiwa ni miezi mitatu tangu Rais Magufuli alipoagiza
mamilioni ya yaliyochangwa kwa ajili ya sherehe ya kumkaribisha Bungeni
kutumika kununua vitanda katika hospitali hiyo, ambapo vitanda 300
vilinunuliwa.
Baada ya kuongea na uongozi wa hospitali hiyo kuhusu
changamoto zinazowakabili pamoja na hatua nzuri waliyoipiga katika
kuhakikisha wanakabiliana nazo, Rais Magufuli aliwaambia wananchi
waliokuwa wakimsubiri nje ya hospitali hiyo kuwa amejifunza mengi
kupitia ziara hiyo na atayafanyia kazi ili kuhakikisha wananchi wanapata
huduma bora zaidi.
“Nimeiona hali halisi mwenyewe. Watu wanapata
shida, watu wana mateso. Na ndio maana nimeamua kuja kwa makusudi
sikuomba ruhusa hapa ili kusudi nijionee hali halisi ilivyo. Nimejifunza
mengi, ninayabeba na najua namna ya kuyatatua. Mungu awabariki sana,”
alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alitumia ziara hiyo pia
kumtembelea Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zuberi ambaye
amelazwa kwenye hospitali hiyo ya Taifa akipata matibabu, na alimfariji.
No comments:
Post a Comment