11 January 2016

CUF yakataa kurudia uchaguzi Zanzibar



4 Mgombea Urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamadi (Cuf), akisoma taarifa yake mbele ya wanahabari (hawapo pichani) katika mkutano wake na vyombo mbalimbali vya habari katika Ukumbi wa Hoteli ya Serena jijini Dar leo.
3Wanahabari wakiendelea kumsikiliza Maalim Seif Sharif Hamadi (Cuf) kwa makini.
5Maalim Seif akiendelea kusoma taarifa yake.
1Mmoja wa wahariri wa chombo kimoja cha habari akiuliza swali kwa Maalim Seif Sharif Hamadi (hayupo pichani) katika mkutano wake na vyombo mbalimbali vya habari katika Ukumbi wa Hoteli ya Serena jijini Dar.
3Mkutano huo ukiendelea.
6Waandishi wa habari na wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakichukua tukio hilo.
7Hali ilivyokuwa.
(PICHA: DENIS MTIMA/GPL)
Hatimaye, Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ametoa msimamo wake na chama chake kufuatia mazungumzo ya siri ya kutafuta suluhu ya mkwamo wa kisiasa unaotokana na tangazo la kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar.
Akizungumza leo na waandishi wa habari katika hotel ya kitalii ya Serena jijini Dar es Salaam, Maalim Seif amesisitiza kuwa hoja ya kurudia uchaguzi wa Zanzibar kama inavyoelezwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), haina msingi, haikubaliki na sio halali kikatiba.
“Hoja ya kurudia uchaguzi haina msingi, haina uhalali, ni hoja ambayo inaweza kuzaa fujo na vurugu na inaweza kuleta mzozo mkubwa wa kikatiba wa kisheria. Sidhani kama tunataka kuwapeleka huko watanzania,” alisema Maalim Seif.
Makamu huyo wa kwanza wa rais wa Zanzibar ameeleza kuwa tayari wameshafanya vikao nane vilivyowashirikisha wagombea urais pamoja na marais wastaafu wa Zanzibar lakini hawakukubaliana kurudia uchaguzi kama baadhi ya viongozi wa CCM walivyoeleza.
Aidha, Maalim Seif amekanusha kilichoelezwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd baada ya kukutana na Rais John Magufuli, kuwa rais alisema warudie Zanzibar kujiandaa na marudio ya uchaguzi kwani rais hakusema hivyo alipokutana naye.
Maalim Seif amesema kuwa ana imani kubwa na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli katika kuleta maridhiano na ufumbuzi wa mgogoro wa Zanzibar kutokana na mazungumzo aliyofanya naye hivi karibuni katika Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa endapo uchaguzi mkuu utatakiwa kurudiwa, zipo changamoto nyingi za kikatiba ambazo zitakwamisha zoezi hilo hivyo uchaguzi huo hautawezekana.
Ametaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na kupitishwa kwa fedha za kugharamia uchaguzi na baraza la wawakilishi ambalo hivi sasa halipo kwa kuwa limefikia ukomo wake.
Mbali na hilo, Maalim Seif alieleza kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu kwa kutoa tamko lisilo halali la kufuta uchaguzi huo huku akifahamu dhahiri kuwa hana nguvu hiyo kikatiba.
Ameitaka ZEC iongozwe na makamu mwenyekiti wake kwa mujibu wa katiba pamoja na wajumbe wengine kukamilisha utaratibu wa kuhakiki matokeo ya uchaguzi na kumtangaza mshindi.
Maalim Seif ameeleza kuwa anafahamu dhahiri kuwa kuna mpango wa kutangaza kwa nguvu marudio ya uchaguzi Februari 28 mwaka huu, lakini yeye pamoja na chama chake hawatakubali.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname