Uchaguzi wa kumpata Meya wa jiji la Tanga umezua vurugu
kubwa leo baada ya Mkurugenzi wa Jiji hilo kumtangaza mgombea wa CCM
kuwa mshindi licha ya chama hicho kuzidiwa idadi na madiwani wa Chama
cha Wananchi (CUF).
Madiwani wa Ukawa wako 20 huku madiwani wa CCM wakiwa 17,
hivyo upande wa UKAWA walikuwa na imani kuwa kwa wingi wao wangeweza
kuongoza Halmashauri hiyo kwa kupata kura nyingi.
Taarifa za kuaminika kutoka katika chumba cha kupigia kura
zimeeleza kuwa baada ya zoezi la kupiga kura, Mkurugenzi na timu yake
walihesabu kura zote zilizopigwa na baadaye alitangaza kuwa mgombea wa
CCM ameshinda kwa kupata kura 19 dhidi ya mgombea wa CUF ambaye amepata
kura 18.
Baada ya tangazo hilo, vurugu kubwa ilizuka ukumbini hapo
huku CUF wakidai kuwa ilikuwa mbinu ya CCM kumtumia Mkurugenzi wa jiji
hilo kuhujumu uchaguzi na kumpa ushindi mgombea wake.
Zoezi la kumchagua Meya wa jiji hilo lilitanguliwa na
uchaguzi wa Naibu Meya ambapo mgombea wa CUF alitangazwa kuwa mshindi
kwa kupata kura 21 dhidi ya mgombea wa CCM aliyepata kura 16, matokeo
ambayo CUF wanadaiwa kuyapinga wakidai yaliandaa mazingira ya hujuma ya
Meya.
“CUF wanadai kuwa Mkurugenzi aliandaa mazingira ili
ionekane kuwa kuna diwani mmoja wa CCM alimpigia kura mgombea wa CUF
kwenye unaibu Meya, ili baadae aoneshe kuwa kuna wagombea wa CUF
waliompigia kura mgombea wa CCM na kumuwezesha kushinda,” Chanzo
kimeiambia Mpekuzi.
No comments:
Post a Comment