Rais
Jakaya Kikwete amesema ukiona Waziri anajisifia kafanya mambo kadhaa
kwa uwezo wake, huyo ana matatizo ya ufahamu na ni mpenda sifa, kwa
sababu mambo anayoyafanya anatekeleza majukumu aliyopewa na Rais na kwa
mujibu wa muongozo aliopewa.Alisema hayo jana wakati akiagwa jijini Dar
es Salaam na taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Ujenzi, huku akiongeza
kuwa vuguvugu za kisiasa zinazoendelea, ni moto wa mabua ambao hauwaki
ukadumu.
Kwa
mujibu wa Rais Kikwete, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli ambaye pia
ndiye mgombea wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), angekuwa kama
mawaziri hao, angejisifia kwa mafanikio yote yaliyopatikana katika
Wizara alizoziongoza, ikiwemo Wizara hiyo ya Ujenzi
Katika
hotuba hiyo amesema sifa moja ya Dk Magufuli ni kutambua kuwa akiwa
Waziri, anafanya kazi kwa niaba ya Rais kwa mujibu wa muongozo na
rasilimali alizopewa, ambavyo vimeeleza nini anatakiwa kufanya kama
waziri.
“Sijawahi
kukusikia ukijisifia binafsi maana na wewe ungeweza kabisa kufanya
hivyo kwa sababu barabara zote hizi ungeweza kusema ni mimi nimejenga na
sio Rais… Sasa bila Rais kukuteua na kukupa muongozo na rasilimali
ungepata nafasi ya kujenga hizo barabara?”
Alihoji
Rais Kikwete. Alisema baadhi ya watu wamediriki kusema waliyoyafanya ni
wao na sio Rais aliyewapa muongozo huo kufanya yoliyofanyika na
kuongeza: “Unadhani Rais atakuja kujenga nyumba? Amekwambia nimekupa
hivi hapa na kila mtu niliyemteua nafanya hivyo na inatangazwa kwenye
gazeti la Serikali.”
Rais
Kikwete alisema Rais hana ushindani na Waziri wake na pia Waziri hana
mashindano na Rais kwa sababu Waziri anafanya kazi kwa niaba yake maana
ndiye aliyemteua.
Moto
wa mabua Alisema CCM imemteua Dk Magufuli kugombea nafasi ya Urais
kupitia chama hicho na ana imani atapita salama kwa sababu ni mtendaji
kazi mzuri na kwamba vurugu zinazoendelea za kisiasa ni moto wa mabua
tu. “Nina imani chama chetu kimekuteua kuwa mgombea wa urais kwa sababu
ni mtendaji… Taifa litanufaika likipata kiongozi kama wewe, hao wengine
ni moto wa mabua tu hauwaki ukadumu,” alisema Rais Kikwete.
Rais
Kikwete alisema ana imani Mungu akijalia Magufuli kuwa Rais basi yale
mambo mazuri aliyoyafanya katika Wizara ya Ujenzi na sekta ulizopata
kuongoza, atatumia maarifa na uzoefu huo kusukuma mbele gurudumu la
taifa mbele. Alisema Dk Magufuli kila wizara aliyopelekwa alifanya
vizuri, ikiwa ni pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Miundombinu na
Ardhi ambapo alisaidia kuondoa ujanja ujanja na kuimarisha nidhamu
lakini hakuwahi kusema ni yeye binafsi ameleta manufaa hayo.
“Kuna
wakati sehemu fulani ina matatizo watu wanasema jamani kwa nini
msimlete Magufuli, tunasema hawezi kuwa kila mahali… Na sekta hii ya
ujenzi ni sekta muhimu na kubwa, nashukuru chini ya uongozi wako
tumeifikisha mahali pazuri,” alisema Rais Kikwete.
Aidha
Rais Kikwete alisema anajivunia kuunganishwa kwa barabara zote za mikoa
na Wilaya nchini katika kipindi cha uongozi wake na hiyo ni kwa
jitihada na usimamizi uliofanywa na Waziri Dk Magufuli.
“Katika
uongozi wangu tumefanikiwa kuunganisha karibu mikoa yote nchini kwa
kiwango cha lami. Jambo hili limewezekana kwa ushirikiano na wafanyakazi
wote pamoja na wataalam wa wizara hii ya ujenzi.”
Kikwete
alisema alipoingia madarakani, bandari ya Dar es Salaam ilikuwa
inasafirisha jumla ya tani milioni 6.7 za mizigo kwa mwaka, lakini hivi
sasa bandari hiyo inasafirisha mizigo zaidi ya tani milioni 15 hadi
mwishoni mwa mwaka huu, bandari ya Dar es Salaam itakuwa na uwezo wa
kusafirisha zaidi ya tani milioni 18, kitu ambacho kitaongeza ukuaji wa
uchumi na kuongezeka kwa pato la taifa.
No comments:
Post a Comment