Dodoma. Jana ilikuwa kama sinema pale viongozi
wa Kamati Namba Moja ya Bunge Maalumu walipojikuta wakibishana na mjumbe
wao mbele ya waandishi wa habari, huku siri za mambo ya ndani ya vikao
zikianikwa hadharani.
Kamati hiyo inaongozwa na Naibu Waziri, Ofisi ya
Makamu wa Rais, Ummy Mwalimu na makamu wake ni Waziri wa Sayansi na
Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, huku ikiwa imesheheni vigogo wengine
wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Viongozi wengine katika kamati hiyo ni Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uhusiano na Uratibu), William Lukuvi, Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika na Waziri wa
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi.
Wamo pia Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk
Seif Rashid, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka na Naibu Waziri
wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Pindi Chana.
Jana asubuhi, Mwalimu na Profesa Mbarawa walifika
mbele ya waandishi wa habari katika Hoteli ya St Gasper wakiwa
wameambatana na mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa
Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy.
Lengo la mwenyekiti na makamu wake lilikuwa ni
kumbana Keissy ili akanushe taarifa aliyoitoa juzi kwenye moja ya
televisheni kwamba kamati hiyo inaongoza kwa kuvunja kanuni hasa katika
suala la akidi ya vikao kutotimia.
No comments:
Post a Comment