21 April 2014

TAULO LA IVO MAPUNDA NA MKONO WA KAVUMBAGU


TANGU mwanzo mambo yalionekana hayaendi sawa kati ya straika wa Yanga, Didier Kavumbagu na kipa wa Simba, Ivo Mapunda, hawakusalimiana kabla ya mchezo uliozikutanisha timu zao juzi Jumamosi Uwanja wa Taifa.

Kavumbagu aliingia uwanjani wakati tayari robo ya wachezaji wa
Simba ikiwa imeshasalimiana na wale wa Yanga tayari kwa kuanza mchezo huo wa Ligi Kuu Bara ulioisha kwa sare ya bao 1-1.

Mapunda anaamini Kavumbagu alimfanyia makusudi kukacha kupokea mkono wake alipomsalimia na kushangazwa na tabia hiyo iliyoonyeshwa na mchezaji huyo raia wa Burundi.

“Yule mchezaji anayeitwa Kavumbagu hakunisalimia wakati tukipeana mikono, sijui ni kwa sababu gani maana sijawahi kumkosea wala kujibishana naye ndani na nje ya uwanja, nakumbuka hakunisalimia nafikiri ni mambo ya ushirikina, labda alidhani nina uchawi,” alisema Ivo.

Ivo alienda mbali zaidi kwa kusema: “Tazama ni Kavumbagu huyo huyo aliyeanzisha sekeseke la taulo langu na kwenda kulitupa kwa mashabiki wa Yanga, imani za kishirikina ndiyo zimewatawala wachezaji, sasa taulo la kujifutia linaingizwaje na imani za kishirikina?”

Hata hivyo Mwanaspoti lilipozungumza na Kavumbagu alisema: “Matukio hayo yalitokea kama bahati mbaya tu, sikuwa na imani yoyote juu ya Ivo.” Alipoulizwa kuhusu kulipeleka taulo kwa mashabiki, Kavumbagu alisema: “Ahaa, nilijisikia tu kufanya hivyo.”

Dakika ya 56 baada ya Yanga kukosa bao la wazi katika lango la Simba huku Mapunda akiwa ametoka langoni.

Yanga ilikosa bao la wazi na kila walipokuwa wakipiga mpira kuelekea wavuni ulikuwa ukizuiwa na mabeki wa Wekundu wa Msimbazi.

Baada ya tukio hilo wachezaji wa Yanga walionekana kutokuwa na imani na taulo lililowekwa nyavuni na Mapunda, ndipo Hamis Kiiza wa Yanga alipotaka kuliondoa mahali hapo lakini akasita, Hassan Dilunga alipolitoa na kulitupa chini. Kavumbagu akaona haitoshi akaliokota na kulitupa kwa mashabiki.

Kocha wa makipa wa Simba, Idd Pazi alipeleka taulo lingine lililokuwa likitumiwa na kocha Zdravko Logarusic, nalo liliondolewa baadaye na shabiki anayedaiwa kuwa wa Yanga.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname