17 October 2013

WALE WANAWAKE WA KINGEREZA WALIOMWAGIWA TINDIKALI ZANZIBAR..!! WATANGAZA KURUDI MWAKANI...!!





Raia wawili wa Uingereza waliomwagiwa tindikali visiwani Zanzibar miezi mitatu iliyopita, wamepanga kurejea tena visiwani humo kuendelea na kazi za kujitolea ikiwemo kuwahudumia watu wasiojiweza. 
 

Raia hao wa Uingereza, Kirstie Trup na Katie Gee, hivi sasa wanaendelea kupata matibabu katika Hospitali za Chelsea na Westminster London na taarifa zinaeleza kuwa afya zao zimeimarika kwa kiwango cha kuridhisha hasa baada ya kufanyiwa upasuaji na kisha kuwekewa ngozi upya. 
Pamoja na madhara waliyokumbana nayo raia hao wamesema kuwa bado hawajakatishwa tamaa na tukio hilo na sasa wanapanga kurejea tena visiwani humo kuendelea na kile walichokiita ‘kazi za upendo’.
 


Katika waraka wake uliochapishwa na Gazeti na Daily Telegraph, Kirstie Trup amesema kuwa yeye na mwenzake wamepanga kurejea Zanzibar mwaka ujao na kwamba safari hii wataongeza kasi ya kushiriki kazi za kujitolea.
 

“Kwa sasa tuko imara na mwakani tumepanga kurejea tena visiwani Zanzibar kushiriki katika kazi za kujitolea,” alisema Trup ambaye ngozi yake imefanyiwa ukarabati wa kisayansi na kuwekewa ngozi upya katika eneo la mkono wa kulia na sehemu ya bega.
 

Akielezea zaidi kuhusiana na tukio hilo la kumwagiwa tindikali, Trup alisema kuwa anachokumbuka ni kuwa wakati akiwa na mwenzie wakielekea mgahawani ghafla walijitokeza watu wawaili na walipowakaribia walichomoa kopo kutoka kwenye mfuko na kumwaga kitu cha majimaji ambacho baadaye kilibainika kuwa ni tindikali.
 

“Mwili mzima uliwaka kama vile nimechomwa na moto. Maumivu yalikuwa makali sana yasiyoweza kuelezeka hasa katika eneo la bega langu la kulia. Nachokumbuka kingine ni kuwa tulipiga kelele kwa sauti sana hata kufanya wale waliokuwa kwenye hoteli iliyokuwa jirani na sisi kutahamaki,” alisema Trup.
 

Amesema kuwa baada ya tukio hilo alijitokeza mtalii ambaye aliwapa msaada kwa kuwamwagia maji sehemu walizojeruhiwa na baada ya hapo walijitosa baharini katika kile walichoeleza ni kujaribu kutuliza maumivu.
 

“Yule mtalii alituonyesha moyo wa ukarimu sana maana alituhudumia vizuri na baadaye tulichojoa nguo zetu na kujitupa baharini kwani maumivu yaliendelea kuongezeka na hali izidi kuwa mbaya maana hata rangi ya ngozi yangu ilianza kubadilika,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname