Dar es Salaam. Serikali imesema mabalozi
wanaowakilisha nchi zao nchini wanapaswa kutambua kuwa, wanawajibika
kuheshimu Mkataba wa Kimataifa wa Vienna unaoainisha taratibu za
diplomasia.
Pia, inasema inajiandaa kumwandikia
barua Balozi wa China nchini, Lu Younqing kutokana na hatua yake ya
kujihusisha na mambo ya siasa.
Wiki iliyopita, Balozi Lu alijitokeza
kwenye mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika mkoani Shinyanga, huku
akiwa amevalia moja ya sare za chama hicho, hatua ambayo imezusha
mjadala miongoni mwa vyama vya siasa na wachunguzi wa mambo ya
kidiplomasia.
Akizungumzia kitendo hicho jana, Naibu
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma
Maalim, alisema Serikali inajiandaa kumwandikia barua ya kumkumbusha
wajibu wake na kwamba itafanya hivyo baada ya kukusanya taarifa zake.
Hata hivyo, Mahadhi alisema Tanzania na
China zitaendelea kuwa marafiki wanaoshirikiana kwenye nyanja mbalimbali
kwa shabaha ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.
“Hizi taarifa za balozi kuwa kwenye
mkutano wa CCM nami zimezisikia na kuziona kwenye vyombo vya habari,
tunachokifanya sasa wataalamu wetu wanaendelea kuzifanyia kazi, baadaye
tutamwandikia barua kumkumbusha wajibu wake,” alisema.
Alisema siyo vyema kwa mabalozi
kushiriki mambo ya kisiasa, kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na
Mkataba wa Vienna ambao ndiyo unaotoa mwongozo.
Pia, Mahadhi aliasa vyama vya siasa
kutoachia majukwaa yao yakitumiwa na wanadiplomasia, akieleza kuwa navyo
vinawajibika kuheshimu mkataba huo.
Alisema iwapo pande zote zitaheshimu mkataba huo, hakutakuwa na kurushiana lawama.
Mwananchi

No comments:
Post a Comment