01 August 2013

MWALIMU MKUU WA SHULE YA CHALINZE AHAMISHIA OFISI YAKE CHOONI


MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Chalinze Mzee, wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, Elias Kapama, yuko katika wakati mgumu baada ya kuhamishia ofisi yake kwenye vyoo vya wanafunzi kutokana na jengo la ofisi yake kuharibika vibaya.


Hatua ya kuhamia chooni ilitokana na mkuu huyo kutawaliwa na hofu ya ubovu wa ofisi yake, hivyo kushindwa kufanya kazi zake kwa ufasaha unapotokea upepo au mvua.


Novemba 2012, Kapama alihamishia ofisi yake katika jengo la vyoo vya wanafunzi ambavyo havijaanza kutumika tangu ujenzi wake ukamilike mwaka 2011.


Akizungumzia hali hiyo, Kapama alisema kuwa anajisikia vibaya kutumia chumba maalumu cha kubadilishia nguo cha wavulana katika choo hicho kutokana na kukosa msaada kutoka halmashauri ya wilaya hiyo.


Alisema kuwa ni miezi tisa sasa tangu ahamishie ofisi yake chooni na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na ngazi ya wilaya pamoja na kufahamu mazingira hayo, hali aliyodai kuwa inamweka katika wakati mgumu.

“Sina ofisi, nimelazimika kuomba kwa wafadhili waliotujengea vyoo kwa ajili ya wanafunzi niweze kutumia chumba hiki cha kubadilishia nguo kama ofisi yangu hadi pale tutakapojenga ama kufanyia ukarabati ofisi ya zamani,” alisema.


Vyoo hivyo ambavyo vimejengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Ebenezer Spritual Center ya mjini Chalinze, vimegharimu kiasi cha sh milioni 70 hadi kukamilika.


Mkuu huyo aliongeza kuwa kwa sasa walimu wanatumia tundu moja la choo huku wanafunzi 450 wakitumia matundu saba, matatu kwa wanawake na manne kwa wavulana.


Hata hivyo mwandishi wetu alishuhudia choo hicho kinachotumika sasa kikiwa hakina hadhi na usalama kwa watumiaji.


Aliuomba uongozi wa wilaya pamoja na wizara ambao umetembelea shule hiyo na kushuhudia mazingira hayo magumu kufanyia utekelezaji wa ujenzi wa ofisi hiyo haraka ili aweze kuhama kutoka chooni.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname