Wakati matukio ya baadhi ya vigogo na
wasanii maarufu wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulenya
hayajapoa, imebainika kuwa mtambo maalumu wa kuchanganya na kuziongezea
thamani dawa hizo upo hapa nchini.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili
zimeeleza kuwa mtambo huo ambao awali ulikuwa unapatikana Mombasa,
Kenya, pekee, unatumika kuchanganya dawa za kulevya na
kemikali nyingine
ambapo nusu kilo ya heroine huongezwa hadi kufikia kilo mbili.
Uchunguzi unaonyesha kuwa kuwa mtambo
huo ulioingizwa mwaka huu na kigogo mmoja wa dawa hizo, upo katika
nyumba moja iliyopo eneo la Mbezi Beach.
Mmoja wa watumiaji wa dawa hizo ambaye
hakutaka kutajwa gazetini kwa kuhofia usalama wake, alisema mtambo huo
umerahisisha upatikanaji wa heroine nchini maarufu ‘white sugar’ kama
inavyojulikana mitaani.
“Zamani ‘white sugar’ ikitoka shamba
(nchi inakotengenezwa yaani Pakistan na nchi nyingine) ilikuwa
inapelekwa Mombasa, Kenya, ambako kuna mtambo wa kuchanganya na dawa
nyingine ili iongezeke wingi wake, lakini kazi hiyo inafanyika hapa hapa
nchini kwa sasa,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu uwepo wa mtambo huo
hapa nchini, Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa
alisema kuwa kuna taarifa alizonazo ambazo bado anazifanyia kazi.
“Hata kama nikiwa nazo nazifanyia kazi, za kwangu mimi nazifanyia kazi na hata za kwako nazifanyia kazi,” alisema Nzowa.
Hata hivyo, Nzowa akizungumza katika
kipindi cha Malumbano ya Hoja kilichorushwa na Televisheni ya ITV juzi,
alisema kuwa katika siku za hivi karibuni wafanyabiashara wa heroine
wamekuwa wakiingiza nchini malighafi za dawa hizo, tofauti na awali
ambapo walikuwa wakiingiza dawa hizo zikiwa tayari kwa matumizi.
Akitoa mfano alisema kuna raia wa kigeni
alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es
Salaam, akiwa na malighafi hizo zilizokuwa zikifanana na sukari na
kwamba Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Mkemia Mkuu wa Serikali,
ndiyo waliobaini kuwa haikuwa sukari kama ilivyodhaniwa.
Alisema kutokana na uhaba wa dawa hizo
bei ya kete imepanda ambapo hivi sasa hakuna kete ya gramu 0.11
inayouzwa chini ya Sh 3,000.
Hii ni mara ya pili kubainika kuwepo kwa
mtambo wa kutengenezea dawa za kulevya nchini. Miaka ya hivi karibuni
jeshi la polisi lilikamata mtambo wa kutengenezea dawa za kulevya katika
nyumba moja iliyopo eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
Uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa
mbali ya kuwepo mtambo huo kuna nyumba tano katika eneo la Tandika
jijini Dar es Salaam karibu na soko, ambazo zinatumika kuuza dawa za
kulevya huku baadhi ya polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, wakiwalinda
wauzaji wake kwa kuwapa taarifa ya mipango inayopangwa na jeshi la
kuwatia mbaroni.

No comments:
Post a Comment