SIKU chache baada ya serikali za
Tanzania na Thailand kutiliana saini mkataba wa kubadilishana wafungwa
na kutekeleza sheria ya vifungo, raia wa Tanzania amebambwa na dawa za
kulevya nchini humo.
Mtanzania huyo aliyefahamika kwa jina
moja la Kileo, alikamatwa Jumanne wiki iliyopita katika kisiwa cha Macau
akiwa amemeza dawa hizo aina ya cocaine akielekea China.
Kwa mujibu wa maofisa wa polisi wa
Thailand, dawa hizo zinakadiriwa kufikia kilogram 1.091, zikiwa na
thamani ya dola za HongKong 900,000.
Waziri Mkuu wa Thailand, Yingluck
Shinawatra, akiwa ziarani nchini alitiliana saini na serikali
kubadilishana wafungwa, jambo ambalo baadhi ya wadadisi wa mambo walidai
ni hatua ya kuwanusuru vigogo waliofungwa huko kwa makosa ya
kujihusisha na biashara hiyo.
Katika mkutano na waandishi wa habari
Jumamosi wiki hii kwenye makao makuu ya polisi, msemaji wa polisi nchini
Thailand alisema wanamshikilia Kileo (37) aliyekamatwa Jumanne 5:30
asubuhi kwenye eneo la kukagua mizigo katika uwanja wa ndege.
“Polisi walimsimamisha baada ya kumtilia shaka na kumweka katika kamera za X-ray ndipo wakabaini kuna kitu tumboni.
Alisema kuwa baada ya kubaini kuwa ana
kitu kisicho cha kawaida tumboni alichukuliwa na kupelekwa kwenye
hospitali ya Conde de Sao Januario kwa uchunguzi zaidi.
Kwa mujibu wa gazeti la ‘The Macau Post
Daily’ la nchini humo lililochapisha habari hiyo, polisi walisema kuwa
mshukiwa huyo aliwaambia kuwa alichukuliwa ili kusafirisha dawa hizo
kutoka mji mmojawapo ulioko Tanzania mapema mwezi huu.
Taarifa zaidi zilisema kuwa mtuhumiwa
huyo awali alipanda ndege kwenda Ethiopia kisha akaenda Thailand mahali
alipomeza dawa hizo na baadaye akapanda ndege hadi kisiwa cha Macau ili
kuelekea Guangzhou mahali ambapo alitarajiwa kuonana na mchora mpango wa
sakata hilo.
Mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani akikabiliwa na makosa ya kusafirisha dawa za kulevya.
Polisi walisema kuwa Kileo aliwaeleza kwamba alilipwa dola za Marekani 7,000 kukubali kumeza na kusafirisha dawa hizo.
Hii ni mara ya pili ndani ya wiki mbili
kwa raia wa Tanzania kushikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumeza na
kusafirisha dawa za kulevya.
Mtuhumiwa mwingine alitokea kusini
mashariki mwa Afrika na kisha kukamatwa na polisi baada ya kuwasili
uwanja wa ndege wa Thailand Julai 10 mwaka huu.
Mtuhumiwa huyo pia aliwaeleza polisi hao kuwa alipita akiwa amemeza dawa za kulevya na kuzisafirisha kupitia njia ile ile.
Polisi bado wanachunguza kama watuhumiwa hao walichukuliwa na kundi lilelile linalosafirisha dawa ya kulevya
Source:Mtanzania Daima

No comments:
Post a Comment