MLIMBWENDE wa East Africa 2010, Anneth Kaguo, Jumatano iliyopita alinusurika kuchezea kichapo kutoka kwa vijana na watoto wanaoishi katika mazingira magumu ‘ombaomba’ katika maeneo ya Mnazi Mmoja jijini Dar.
Tukio hilo lilitokea saa moja usiku na kushuhudiwa na mwandishi wetu baada ya mlimbwende huyo kujikusanya na kwenda maeneo hayo kwa lengo la kutoa msaada kwa vijana na watoto hao wanaojitafutia riziki zao mitaani.
Tofauti na matarajio yake, baada ya mrembo huyo kufika eneo hilo aliwakuta vijana na watoto hao wakiwa wachache, hata hivyo aliamua kuwapa nasaha za maisha kabla ya kuwapa alichowapelekea.
Ghafla, kundi lingine la vijana hao liliibuka na kujichanganya na wenzao hasa baada ya kusikia kwamba kulikuwa na msaada utakaotolewa.
Anneth alipomaliza kutoa nasaha zake, alianza kugawa vitu alivyovibeba ikiwa ni pamoja na nguo, sabuni na sukari.
Songombingo lilianza mara baada ya kumaliza kugawa misaada ambapo baadhi ya vijana na watoto hao walianza kulalamika kuwa vitu hivyo havikuwa na ubora halisi na kwamba alitumwa na Freemason.Wakaanza kumzonga na kumwambia watamkomesha.
Makelele yaliyoambatana na kuzomea, huku wengine wakitishia kuvunja vioo vya gari lake, yaliwafanya watu wengi kusimama na kutaka kujua kinachoendelea.
Baada ya vijana hao walizidi kuja juu na kuanza kumtia masingi mrembo huyo, akaamua kukimbia.
Anneth alifanikiwa kuingia ndani ya gari lake na kuondoka kwa kasi eneo hilo huku akiapa kutorudia tena kutoa misaada kiholela.
“Ni heri ningeenda katika kituo cha watoto yatima,” alisema.
No comments:
Post a Comment