09 September 2012

uwezekano wa TFF kuifungia Simba kusajili miaka miwili





KAMA Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), likisimama kwenye kanuni za usajili basi Simba ina hatari ya kufungiwa kusajili kwa miaka miwili kama itapatikana na hatia ya kumsajili Ramadhan Chombo 'Redondo' wakati akiwa na mkataba na timu yake ya zamani, Azam FC.


Ingawa beki Kelvin Yondani anaweza kuingiza Yanga kwenye mkumbo huo wa kufungiwa, suala lake liko tofauti kidogo.

Suala la usajili wa Redondo ni miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kuamuliwa na Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF, itakayokutana chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa keshokutwa Jumatatu.

Usajili wa Redondo umewekewa pingamizi kwani ana leseni ya kuchezea Azam kwa msimu wa 2012/23.

Ingawa Simba na Azam, zimemalizana kuhusu suala la Redondo, inadaiwa kuwa mambo yanaweza kubadilika Jumatatu kwani kamati ya Mgongolwa inataka kusimamia taratibu, badala ya kumalizana mambo nje ya sheria.

Pia mkataba wa Redondo na Azam unasemekana unamalizika mwaka 2013.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya TFF zinaeleza vigogo wake wamepania kusimamia katika kanuni ili kuhakikisha kuwa matatizo yote ya usajili yanamalizika kwa mujibu wa kanuni za TFF au zile za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Pamoja na kanuni za TFF kutobainisha adhabu kwa timu inayosajili mchezaji, ambaye ana mkataba na timu nyingine lakini kanuni za Fifa ziko bayana na suala hilo.

Kanuni ya 43 ya masuala ya usajili ya TFF inaeleza kuwa klabu inayotarajia kuingia mkataba na mchezaji wa kulipwa haina budi kuiarifu klabu yake ya sasa kwa maandishi kabla ya kufanya makubaliano na mchezaji huyo. Kinyume cha hapo inatakiwa kutolewa adhabu, ambayo haijabainishwa na hapo ndipo kanuni za Fifa zinapoingia.

Vifungu vya tatu na nne vya kanuni ya 17 ya Kanuni za Usajili na Uhamisho za Fifa zinaeleza bayana kuhusu timu kutoruhusiwa kusajili kwa misimu miwili kama itahamisha mchezaji mwenye mkataba bila kuhusisha klabu ya pili.

Pamoja na klabu husika kupigwa faini, mchezaji mwenyewe anatakiwa kufungiwa kucheza soka miezi minne ikiwa itabainika amehusika na kitendo hicho.

Chelsea ya England iliwahi kuonja joto ya jiwe ya kanuni hiyo mwaka 2009 baada ya kufungiwa wakati walipomsajili Gael Kakuta kutoka Lens ya Ufaransa ingawa walikata rufaa na kushinda kwenye Baraza la Usuluhishi wa kesi za michezo.

Pamoja na kuwapo kwa pingamizi nyingi kwenye Kamati ya Mgongolwa, masuala mengine yanayosubiriwa kwa hamu ni pamoja na lile la Yanga kumsajili Yondani, ambaye mkataba wake na Simba ulimalizika Mei, 2012.

Yanga ilimsajili Yondani akiwa mchezaji huru ingawa kuna utata wa suala hilo kwani timu yake ya zamani ya Simba inadai ana mkataba mwingine ambao aliongeza Desemba mwaka jana.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname