KATIKA
mapenzi kuna mambo ambayo hayastahili kupewa muda wa kuyajadili. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba, mengine yanaweza kutibua furaha iliyopo na
kuweza kupindisha maisha yenu.
Kwa kuthibitisha hilo, sikia kisa
hiki. Jamaa mmoja aliyefahamika kwa jina la
Rashid alibahatika kumpata
mke mzuri sana aliyefahamika kwa jina la Wahida. Yaani mwanamke ambaye
kila mwanaume akimuona ni lazima atamani kuwa naye.
Baada ya
mwanaume huyo kumuoa, waliishi kwa muda mrefu sana na ndoa yao ilikuwa
ikitawaliwa na furaha siku zote. Wakabahatika kupata watoto wawili.
Hakika mwanamke huyo alikuwa mke kwa maana halisi ya mke.
Alikuwa
akimheshimu sana mumewe na kumpatia kila aina ya furaha. Kwa kifupi
ilikuwa ni ndoa ya kuigwa. Siku moja Rashid alikutana na rafiki yake wa
muda mrefu sana.
Mazungumzo yao yalikuwa mengi lakini ikafika mahali
yule rafiki akamuuliza Rashid kama ameshaoa. Rashid akajibu kuwa kamuoa
msichana mmoja anayeitwa Wahida. Yule jamaa akashangaa kusikia Rashid
kamuoa Wahida, mwanamke ambaye siku za nyuma alikuwa ni changudoa.
Rashid
aliposikia kuwa Wahida alikuwa changudoa, ati akaumia sana na akaanza
visa kwa mkewe na hatimaye wakaachana. Akaoa msichana mwingine dogodogo
kutoka kijijini ambaye hajaguswa. Alichokiona kwenye ndoa yake hiyo ya
pili alijuta hadi akamkumbuka Wahida.
Tunajifunza nini kwenye kisa
hiki? Ni kwamba, unapokutana na mpenzi wako kwa mara ya kwanza kuna
mambo ya msingi ambayo kiukweli unastahili kuyajua. Hapa namaanisha
historia ya maisha yake. Unapotaka kujua historia ya maisha ya mpenzi
wako siyo lazima kila kitu ujue. Mengine yaache abaki nayo kwani hata
akikuambia hayawezi kukusaidia kiviiile.
Lipo hili swali la umeshwahi
kutembea na wanaume/wanawake wangapi hadi leo? Hili si zuri kumuuliza
mpenzi wako. Kwa nini nasema hivyo? Nina sababu mbili. Kwanza ni vigumu
sana kupata jibu la kweli, yaani tarajia kudanganywa. Hapo unaweza hata
kuambiwa hajawahi kuwa na mpenzi kumbe katika ukweli tangu ameyajua
mapenzi, ametoka nao zaidi ya kumi.
Sababu nyingine ya kwa nini
hustahili kuuliza swali hilo ni kwamba, inaweza kukufanya ukabadili
mawazo yako na hata uhusiano wenu ukakomea hapo. Unaweza kukutana na
msichana mzuri sana mwenye kila sifa nzuri na katika historia yake ya
mapenzi anaweza kuwa ameshapita kwa wanaume kibao kiasi kwamba hata
idadi amesahau.
Sasa kama utamuuliza na yeye akawa mkweli kwako kwa kukujibu kuwa, ni wengi kiasi kwamba hata idadi hakumbuki, utajisikiaje?
Hakika
unaweza kujikuta unanyong’onyea na kushangaa hata ile hamu ya kuendelea
kuwa naye inaisha licha ya kwamba hukustahili kuwa hivyo. Matokeo yake
unaweza kumkosa mtu ambaye alistahili kuwa na wewe na mkaishi maisha ya
raha mustarehe.
Kuwa na idadi kubwa ni tatizo?
Kuna
mtaalam mmoja aliwahi kusema kuwa, katika maisha ya sasa hakuna
mwanamke anayeolewa akiwa na usichana wake na kama wapo ni wachache
sana. Akaeleza kuwa, msichana akishatolewa usichana wake hata akiwa
ametembea na wanaume ishirini hana tofauti na yule aliyetembea na wawili
tu.
Mtaalam huyo akasema, tena inawezekana aliyetembea na wengi
akatulia kwenye ndoa yake kuliko yule aliyetembea na mmoja au hajaguswa
kabisa. Hapo ndipo inapoonekana kwamba, kuwa na historia ya kwamba
uliwahi kutoka kimapenzi na wanaume/wanawake wengi, hakuna madhara
makubwa katika ndoa.
Ndiyo maana inashauriwa kulifutilia mbali swali
la kutaka kujua idadi ya wapenzi aliyowahi kuwa nao huyo mpenzi wako au
hata kuwajua kwa majina. Hii ni kwa sababu hata ukijua haitakusaidia
chochote zaidi ya kukuchanganya na kukufanya ukose imani kwa mpenzi
wako.
No comments:
Post a Comment