INAUMA kusalitiwa, inavunja moyo kuwa mwenzi mwenye hulka za ubinafsi.
Unajitahidi kuwa mwaminifu lakini yeye anakwenda kugawa penzi pembeni.
Wengine wanaita ‘nje cup’. Unajihimu kushirikiana naye ila yeye anataka
afanye mambo yake kivyake.
Kimsingi inauma lakini ndiyo changamoto zilizopo kwenye mapenzi.
Uaminifu umekuwa tatizo,
kwa hiyo unahitaji kujengwa ili hali hiyo
isikutese. Ukimbaini amekusaliti ujue njia sahihi za kupita kukabiliana
na maumivu. Hii ni tiba kamili.
JIFUNZE KUDHIBITI HISIA
Unaposoma makala haya, pengine upo kwenye mateso yanayotokana na
maumivu ya kusalitiwa na mwenzi wako au anakuumiza kwa tabia yake ya
ubinafsi. Hiyo inakufanya uwe na ujazo mkubwa kichwani wa hisia hasi
ambazo zinajumuisha yafuatayo;
* Hasira
* Huzuni
* Wasiwasi
* Fedheha
* Maumivu makali kiakili
Kitu sahihi cha kwanza ambacho unatakiwa kufanya ni kuhakikisha
unaondokana na maumivu ya kiakili ambayo yanasababishwa na kumbukumbu
mbaya za kusalitiwa au matendo yasiyo ya furaha kutokana na jinsi
mwenzi wako anavyoonesha ubinafsi.
Baada ya kuondokana na maumivu ya kiakili unaweza kuamua nini cha
kufanya kuhusiana na hatma ya uhusiano wako. Inawezekana kupima uzito
wa kosa na kufikia mwisho, hivyo ukaachana na mwenzi wako, iwe mchumba,
mke au mume.
Unaweza pia kuamua kuketi meza moja na kumaliza tofauti zenu. Ni sawa
kwa kile ulichoamua lakini lengo hapa ni kuhakikisha kwamba kumbukumbu
za usaliti zinaondoka. Isije mkasameheana halafu siku nyingine katika
mazungumzo ukakumbusha: “Unakumbuka siku ile nilikufumania
nikakusamehe?”
Ni kosa kuchukua uamuzi lakini wakati huo huo ukabaki na kumbukumbu za
tukio la kusalitiwa na mwenzi wako. Iwe unaamua kuachana naye au
mnaendelea, hakikisha hubaki na hasira, huzuni, wasiwasi, kujihisi
fedheha, kudhalilishwa wala husumbuliwi na maumivu makali kiakili.
Baada ya kuhakikisha hilo umelifanikisha zingatia yafuatayo;
PUUZA NA UYAONDOE MAUMIVU YA KIAKILI
Fikiria kama kuna kitufe kama kwenye kompyuta au simu ambacho
ukikibonyeza na maumivu yote yatakwenda na maji. Hivyo basi, unatakiwa
uamini kuwa kila kitu kinawezekana, kwa hiyo hupaswi kusumbuliwa na
mawazo.
Watu wengi ambao wapo kwenye uhusiano wa kimapenzi na watu ambao ni
wasaliti au wabinafsi, wanakabiliwa na maumivu makali ya kihisia. Watu
hao wanatamani kusukuma kitufe cha kuwandoa kwenye maumivu lakini kwa
bahati mbaya, hicho kitufe hakipo.
Kuna njia ambayo ni sawa na kubonyeza kitufe cha kuondoa maumivu. Ni
muhimu kwanza kutambua chanzo cha maumivu. Ukikatiza mitaani, hakuna
hata mmoja ambaye anaweza kuhisi maumivu uliyonayo akilini mwako.
Rafiki zako wanaweza kuwa wanajua kwa sababu umewaambia, pamoja na
hivyo hawawezi kuwa na utambuzi halisi juu ya kile kinachokutesa. Ni
wewe peke yako ambaye unajua kila kitu kuhusu maumivu yaliyomo ndani
yako.
Ukiweza kulitambua hilo, maana yake ni kuwa utakuwa umepiga hatua kubwa
kukaribia kitufe cha kuondoa maumivu yanayokukabili. Umeshakaribia
lakini hujafikia. Jambo muhimu kufanya ni kuondoa hisia hasi. Ukiwa
mbali na hisia hizo, maana yake umepona.
No comments:
Post a Comment