TUNAPENDA
kuongozwa na fikra zetu. Kila mmoja anataka mwongozo wa maisha yake
uendane na halmashauri ya ubongo wake. Hufanya hivyo, bila kujua kuwa
kuna kikomo fulani ndani yake. Akili
na matakwa ya moyo, wakati mwingine
vinaweza kukupoteza.
Moyo unaweza kumpenda mchawi na ukawa huelewi kitu kwa chochote
utakachoambiwa. Penzi la jambazi likikuingia, serikali ndiyo utaiona ni
katili kwa sababu inamsaka mwenzi wako usiku na mchana. Hii ina maana
kuwa mapenzi ni zaidi ya fikra za kila mtu.
Hutokea watu kuachana wakati bado wanapendana. Migogoro midogo
inawafanya watengane, matokeo yake kila mmoja anabaki akiumia kivyake.
Huo ni mfano mmoja kati ya mingi inayoonesha kwamba mapenzi yapo juu ya
fikra za kawaida. Inahitaji utulivu wenye mashiko ya sayansi ya
saikolojia.
Kuna ambao waliishi kwa mategemeo ya kuachana. Wakiamini wamechokana,
matokeo yake kwenye ubongo wao wakatengeneza maneno: “Ipo siku.” Hata
hivyo, miezi na miaka ikakatika mpaka wakazikana. Kumbe Mungu
aliwaandikia wawe pamoja mpaka kifo ila wao hawakujua.
Dosari ya aina hiyo inatokana na wawili wanaopendana lakini upendo wao
ukapofushwa na migogoro ya hapa na pale. Nasisitiza kuwa watu ni lazima
wagundue mapema matatizo yao kabla ya kuhisi kwamba kati yao hakuna
mapenzi. Vilevile, kila mmoja amuelewe mwenzi wake ni binadamu na siyo
malaika.
Ana mapenzi naye, tena mapenzi makubwa. Hata hivyo, hiyo haimfanyi awe
malaika. Ni binadamu, kwa hiyo wakati anadumisha mapenzi yake, anaweza
kufanya makosa mengi. Jaribu kumvumilia kwa sababu ameumbwa na udhaifu,
hajakamilika.
Baada ya utangulizi huo, ni vizuri kujua kuwa yapo makosa ambayo wengi
huyafanya, tena mara nyingi bila kujua. Tunaishi nayo, matokeo yanakuwa
ni mazoea. Hata hivyo, mara nyingi hutokea yanaharibu uhusiano ndiyo
maana nimechagua tuyajadili. Yafuatayo ndiyo makosa yenyewe:
KULICHEZEA KAMARI PENZI LAKO NA MAISHA YAKO
Hapo ulipo hujawahi kuona mtu anapambana kuhakikisha mwenzi wake
anabadilika tabia? Bila shaka tayari ulishajionea. Je, umejifunza nini
kutoka kwao? Ni kweli kabisa kwamba mwenzi wako si malaika, kwa hiyo
mnapokutana lazima mtatofautiana, je, ikitokea hamuendani kabisa?
Umejitahidi kumuweka kwenye mstari unaotaka lakini mwenzako haendi.
Unasubiri nini? Kung’ang’ania penzi la mtu ambaye huendani naye, ni
sawa na kuuchezea kamari moyo wako, vilevile ni sawa na kuyachezea
karata tatu maisha yako.
Upo na mwenzi wako ambaye hakutoshelezi. Mnakutana mara nyingi lakini
hakufikishi pale unapotaka upelekwe na mwandani wako. Unanyamaza tu kwa
imani kuwa ipo siku ataweza, siku zinakwenda na mabadiliko
hayaonekani. Unajipa matumaini kedekede kwamba kuna siku nyoka ataota
miguu na jongoo atakuwa na macho.
Unakuwa na mpenzi ambaye kila siku anakupa visingizio ili msikutane
faragha. Je, kwa nini usijiongeze kwamba mtu huyo hana hisia na wewe?
Au, kwa nini usijiulize kama pengine mtu wako yupo kwenye uhusiano wa
pembeni ambako anatoshelezewa mahitaji yake?
Tatizo kubwa ambalo inatakiwa lijulikane ni kwamba wengi wanapoingia
kwenye uhusiano, hawapimi watu wao ni wazuri kwao kiasi gani. Wanavutwa
na matamanio ya juu. Mvuto wa juu, huipumbaza akili na kudhani moyo
unapenda kumbe ni uongo mtupu.
Mtu anaweza kudumu na mwenzi wake ambaye hamtoshelezi kwa miaka mingi.
Anapumbazwa na mvuto wa juu, kwa hiyo anashindwa kuelewa mantiki ya
muungano wa nyoyo. Zingatia kwamba mwenzi wako ambaye nyoyo zenu
zimeungana, lazima atakuridhisha, naye ataridhika kwa huduma unayompa.
MFANO: Jayden Brown anatoa ushuhuda: “Nikifikiria uhusiano wangu
uliopita nabaki najishangaa. Nilikuwa mbinafsi, nilikuwa naoneshwa
upendo na wapenzi wangu lakini nilikuwa sitoi ukilinganisha na wao.
Nilishangazwa na wanawake waliojitoa kwangu, wao waliamini kuna siku
ningebadilika.
“Wanawake niliokuwa nao, walijipa matumaini kuwa ni muda tu, kipo
kipindi ambacho kingefika na maisha yetu yangekuwa salama. Kumbe
walichowaza wao, hakikuwa ndani ya akili yangu.
“Wao waliamini kwamba upo muda wa mabadiliko ya mimi kuwa mtu bora,
ningebadilika kuwa mwema kwenye mapenzi, ningekuwa mpenzi bora. Kitu
mapenzi juu yao hakikuwa ndani yangu kabisa.”
No comments:
Post a Comment