20 September 2012

HAWA ndo.... MAJAJI usaili wa video ya Diamond


MSANII wa Kimataifa wa Tanzania, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ ataongoza jopo la majaji wengine wanne kwa ajili ya kupata wasichana na wavulana watakaoshiriki kwenye video yake mpya.
Usaili wa watu hao utafanyika Jumamosi kwenye ukumbi wa
Nyumbani Lounge, mjini Dar es Salaam ambao wote watakaochaguliwa kuonekana kwenye video hiyo itakayorekodiwa na kampuni ya I-View Studios watalipwa.
Katika orodha hiyo, yupo mbunifu wa mitindo wa kimataifa, Ally Rehmtullah ambaye hivi karibuni alizundua mavazi yake mapya katika hoteli ya Serena, yupo pia Raqey Mohamed ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya I-View Studios,pia Creative Director, Sammy Cool ambaye ni mwalimu wa dansi na blogger maarufu Missie Popular.
Akizungumza mjini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa kampuni ya One Touch Solutions, Petter Mwendapole alisema majaji hao wamechaguliwa kutokana na kuhusika kwao na shughuli za sanaa kila siku.
“Diamond ndiye mwenye video na ni mwanamuziki, Raqey ndiye atakayerekodi video, lazima ajue watu ambao ana wataka kwenye hiyo video, ameshafanya kazi kama hizi mara nyingi, ni mpiga picha wa kimataifa, Sammy Cool ni densa maarufu na mwalimu ambaye amewafundisha watu wengi katika ulimwengu wa kucheza nchini, wengi watakuwa wakimfahamu tangu enzi za Bombeso, THT na mashindano mbalimbali ya urembo, amekuwa pia akitoa ushauri nasaha.
“Kwa upande wa Ally ni mbunifu wa mitindo wa kimataifa, ameshafanya kazi mpaka ulaya, ana uzoefu mkubwa kutokana na kazi zake kwa hiyo kuwepo kwake kutasaidia pia vipaji vingine kuonekana, Missie Popular yeye ni mwandishi, mwanamitindo kwa hiyo kama mtu wa habari ana mchango wake katika kuibua vipaji pia,” amesema.
Mwendapole amesema usaili huo utaanza saa tano kamili asubuhi na kwamba baada ya usahili huo wale watakaochaguliwa watafahamishwa mazoezi yatakuwa wapi na baada ya hapo kazi ya kurekodi video hiyo kuanza.
Video hiyo ambayo wote watakaochaguliwa kuonekana watalipwa, itarekodiwa maeneo mbalimbali nchini pamoja na sehemu nyingine nje ya bara la Afrika ili kuipa ladha tofauti. Kampuni ya I-View ndio imeshinda mchakato wa kurekodi video hiyo.
Tayari kampuni hiyo imeweza kutengeneza video kadhaa za kiwango cha kimataifa ikiwemo Kwasakwasa Tazneem, Utanikumbuka ya Suma Lee pamoja na matangazo mbalimbali ya biashara. I-View pia ndiyo inatengeneza kava za wasanii mbalimbali Bongo Movie ambao wanafanya kazi na Steps Entertainment.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname