18 July 2012

Cheka aapa hatopigana na Watanzania

BONDIA Francis Cheka, ameapa kwamba hatopanda ulingoni tena kucheza na mabondia wa Tanzania huku akidai pambano lake na Karama Nyilawila la Septemba 29, mwaka huu ndiyo litakuwa la mwisho.

Mabondia hao watapanda ulingoni kuwania ubingwa wa UBO katika pambano la uzito wa kg. 75 raundi 12.

Pambano hilo litasimamiwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST) litakalofanyika katika Ukumbi wa PTA, Dar es Salaam.


Katika pambano hilo kutakuwa na mapambano utangulizi 12 kutoka kwa mabondia chipukizi. 

Akizungumza kwa simu jana, Cheka alisema pambano lake na Nyilawila anaamini litakuwa ni kubwa na lenye msisimko kwani wote wote na uwezo mkubwa na wanarekodi nzuri katika michezo ya kimataifa.

Alisema kutokana na uzito wa pambano hilo ndiyo maana aliamua kusaini mkataba na promota moja kwa moja, ingawa alikuwa ameshakataa kupigana hapa nchini kwa kuwa mobondia wote hawana hadhi na viwango vyao kuwa chini hivyo kuhofia kuvuruga rekodi yake.

"Nitapigana na Nyilawila na nipo tayari kwani natambua uwezo wake ni mkubwa, licha ya kuwa nilishawahi kumpiga kwa pointi katika pambano letu tulilocheza Morogoro lakini nasema hili la sasa ndiyo litakuwa la mwisho kucheza na mabondia wa hapa nchini," alisema.

Aliongeza kuwa kwa sasa anaendelea kujifua kwa ajili ya pambano hilo, kwani anajua anamuda mrefu wa kujiandaa na anaahidi kuchukua ubingwa huo.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname