BONDIA
Francis Cheka ‘SMG’ kutoka Morogoro, kwa mara ya tatu mfululizo usiku
huu amempiga mpinzani wake Mada Maugo kwa Technical Knockout (TKO)
raundi ya saba katika pambano lililokuwa la raundi 12, kwenye ukumbi wa
PTA, Saba Saba, Dar es Salaam.
Maugo
baada ya kupigwa ngumi nyingi katika raundi tatu mfululizo, kiasi cha
kutabiriwa kukaa chini wakati wowote, mwanzoni mwa raundi ya saba
hakurejea ulingoni.
Msaidizi wake, Karama Nyilawila alitupa taulo ulingoni akisema bondia wake hataendelea na pambano.
Refa John Shipanuka kutoka Zambia aliyelimudu pambano hilo, alimuinua mkono Cheka kumtangaza mshindi kwa TKO raundi ya saba.
Baada
ya hapo, Maugo aliinuka kwenye kona yake na kwenda kumkumbatia Cheka na
kocha wake, akisema kwamba amesalimu amri baada ya kuishiwa pumzi.
“Pumzi
imekata, siwezi kuendelea,”alisema Maugo ambaye leo alionekana
muungwana ingawa hakuwa tayari kusema atahitaji pambano la nne au la.
Akiwa
mwenye furaha, Cheka alisema kwamba anamshukuru Mungu amemuwezesha
kuendeleza ubabe wake kwa mabondia wa Tanzania na sasa anageuzia makali
yake kwa Japhet Kaseba ambaye naye ameomba pambano la marudiano.
Katika
pambano la leo, refa Shipanuka alimdhibitu Maugo mwenye desturi ya
kuwakumbatia wapinzani wake ili kukwepa kupigwa na pia kupumzikia kwenye
miili yao.
Kila
alipokuwa akimkumbatia Cheka, Shipanuka alikuwa akifika na
kuwaachanisha na kufanya mabondia hao watumie muda mwingi kupigana.
Pamoja
na hayo, Maugo alilianza pambano hilo vizuri na katika raundi ya pili
almanusra ashinde kwa Knockout (KO) baada ya kumkalisha mpinzani wake
kwa ngumi kali.
Lakini SMG aliinuka na kuendelea na pambano, ingawa limchukua hadi raundi ya nne kuanza kuutawala mchezo.
Raundi
ya kwanza hadi ya tatu, Maugo alifanya vizuri, lakini baada ya hapo
mambo yalikuwa magumu na tangu hapo wengi walijua angepigwa wakati
wowote.
Katika
mapambano ya utangulizi, mdogo wake Cheka, Cosmass Cheka alipigwa kwa
pointi na Sadiki Momba katika pambano la uzito wa Light, wakati Hajji
Juma alimpiga kwa pointi Emmilio Naffat uzito wa bantam.
Simba
Watunduru alimpiga kwa KO raundi ya sita Mohamed Kashinde katika
pambano la uzito wa Feather, wakati Amos Mwamakala alimpiga kwa pointi
Said Muhiddin uzito wa Light.
Moro
Best alimpiga Nassib Ramadhan kwa TKO raundi ya nne uzito wa Bantam na
Salima Kabombora alimpiga Asha Ngedere kwa pointi uzito wa Bantam.
SOURCE-SHAFII DAUDA
No comments:
Post a Comment