Shirika la ndege la Etihad limezindua rasmi mpango
wake wa kuzifikia jamii nchini Uganda ambapo wametoa misaada ya tiketi za
ndege, mablanketi na vifaa vya shule kwa kituo cha kulea watoto “Whisper
Children’s Home” kilichopo Mutai, wilaya ya Jinja, Uganda.
Kituo hicho cha watoto kilianzishwa Mei 2011 lengo
kuu likiwa ni kuboresha maisha ya watoto walioathirika kwa utapiamlo na wanaoishi
katika mazingira hatarishi kijijini hapo.
Akitoa maoni yake juu ya msaada walioupata kutoka
Shirika la ndege la Etihad, Bi. Veronika Cejpkova, Mwanzilishi na Mkurugenzi wa
kituo hicho alisema: “Tunashukuru kwa moyo wa ukarimu uliooneshwa na shirika la
ndege la Etihad. Tiketi hizi zitasaidia sana katika kuwasafirisha wanaojitolea
na wafanyakazi kutoka Ulaya wanaoamua kushiriki na sisi katika shughuli zetu za
kila siku hapa kituoni.
“Mpaka sasa tunawatunza watoto takribani 30.
Mahitaji yao ni pamoja na matunzo, vifaa vya shule kama vile kalamu za wino,
kalamu za rangi na vitabu ambavyo vitawasaidia watoto katika masomo na kuwaburudisha.”
Shirika hili la ndege limetoa msaada huu chini ya
mpango wake wa uwajibikaji kwa jamii uitwayo “Giving Together” unaohusisha
programu mbalimbali zinazotoa misaada kwa wahitaji waliopo katika mtandao wao
duniani.
Toyin Alaran, Meneja Mkuu wa shirika la ndege la
Etihad, Uganda, alisema: “Shirika letu limejikita kuleta maendeleo na kusaidia
jamii zilizopo katika mtandao wetu. Tumeona kituo cha watoto cha Whisper kama
mwangaza wa matumaini kwa watoto na familia zenye kuishi katika mazingira
magumu na tumefurahi kupata nafasi ya kushirikiana nao katika hili.
“Msaada huu kutoka Etihad unadhihirisha msimamo
wetu wa kuunga mkono mipango inayolenga kuleta maendeleo katika jamii na
kuboresha maisha ya wanajamii katika sekta mbalimbali kama elimu kwa watoto na
kuboresha hali ya maisha ya wasiojiweza,” alisema Bw. Alaran.
Etihad ilikabidhi zaidi ya mablanketi 200 kwa kituo
hicho cha watoto. Waliosindikiza katika ugeni huo ni pamoja na; Toyin Alaran,
Meneja Mkuu wa Etihad, Uganda, Maclynn Kemigisha, Mratibu Masoko wa Etihad, Uganda,
Luzelle Boado-Berger, Afisa wa Mipango Endelevu wa Etihad na wanachama watano
wa mpango wa “i Volunteer” wa Etihad, waliowasili Uganda kutoka makao makuu ya
Shirika hilo huko Abu Dhabi ili kuungana na wenzao katika kutimiza azma hii.
Tangu kuanzishwa kwake, timu ya Whisper imetoa
huduma ya kwanza na msaada kwa watoto zaidi ya 2000 waliathiriwa na funza na
imeboresha sehemu za kulala za watoto wa kijiji cha Mutai na vijiji vingine
kanda ya Busoga kwa kuwapa vitanda, magodoro, vyandarua, mablanketi na mashuka.
Whisper pia imezipatia
familia mafunzo ya jinsi ya kuandaa chakula, usafi wa mwili na uzazi wa
mipango, imewafundisha wazee jinsi ya kukarabati nyumba zao, au kutunza bustani
ya mbogamboga, imewapa watoto usafiri wa kwendea shule, na chakula na kuni kwa
familia zinazopitia kipindi kigumu wakati wa mvua kali.
No comments:
Post a Comment