01 December 2015
Huku ndiko yalikopelekwa Makontena Yaliyokwepa Kodi, Kova kutoa Tamko leo
Sakata la upotevu wa makontena 349 kwenye nyaraka za TRA limeendelea kushika kasi huku wahusika wakiendelea kuugua matumbo kufuatia uchunguzi unaendelea.
Taarifa za awali zimeeleza kuwa baadhi ya mizigo iliyopita kwenye makontena hayo ilipelekwa na kushushwa katika baadhi ya maduka makubwa katika soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Tayari serikali imenzisha uchunguzi mkali na makini ili kuwanasa wahusika waliokwepesha Makontena hayo yenye thamani ya shilingi bilioni 80, yasilipe kodi.
Maafisa nane wa TRA ikiwa ni pamoja na aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Rashid Bade wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi, kufuatia amri ya Rais John Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Akiongea na mwandishi wa habari wa gazeti la Mtanzania, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema kuwa leo atatoa taarifa ya ufafanuzi kwa vyombo vya habari.
“Nitatoa taarifa kwa vyombo vya habari ambayo ndiyo itakayofafanua kila kitu, “alisema.
Duru zinaelezwa kuwa maafisa kadhaa wa TRA na Bandari (TPA) wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kama alivyoagiza waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, TRA iliiandikia barua Kampuni ya Said Bakhresa na kusimamisha upelekaji wa makontena kwenye bandari yake ya nchi kivuko (ICD) baada ya kubainika kuwa baadhi ya makontena yalipitia kwao.
Kupitia barua yake kwa kampuni hiyo, TRA ilieleza kuwa kampuni hiyo ilivunja sheria ya forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuruhusu kuondolewa kwa makontena hayo bila kulipa kodi.
Kampuni hiyo ya Bakhresa imetoa ufafanuzi na kueleza kuwa makontena yalipotea hayakuwa mali ya kampuni hiyo. Imeeleza kuwa Inaendelea kushirikiana na polisi kama ilivyoagizwa kuwabaini wamiliki wa makontena hayo ili wachukuliwe hatua sitahiki.
chanzo - dar24
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment