23 November 2015

Mmoja wa Watano Waliookolewa Mgodini Baada ya Kufukiwa Kifusi Kwa Siku 41 Afariki Dunia


MMOJA wa majeruhi watano waliokuwa wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama kutokana na kufukiwa na kifusi cha mchanga na kukaa siku 41 chini ya mgodi na kuokolewa, Onyiwa Kaiwao (55) amefariki dunia.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Joseph Ngowi amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kusema kuwa chanzo cha mauti hayo ni kutokana na majeruhi huyo kutapika akiwa amelala hali ambayo ilifanya matapishi hayo kuingia katika njia ya hewa.

Dk Ngowi alisema Kaiwao alifariki jana saa sita mchana na kuongeza kuwa pia alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa nimonia unaosababishwa na baridi kali hali iliyomfanya kutokuwa katika hali ya kawaida tofauti na wenzake.

Hata hivyo, Dk Ngowi alisema majeruhi huyo pia alikuwa na matatizo katika utumbo, na hivyo kila akienda haja kubwa alikuwa akitoa magome ya miti waliyokuwa wakiyatumia kama chakula wakati wakiwa chini ya ardhi.

Jana (juzi) tuliwachukua vipimo waathirika wote watano na kuonesha kuwa hali zao ni nzuri, lakini Onyiwa alionesha kutokuwa na maendeleo mazuri tofauti na wenzake na ghafla akiwa amelala alijitapikia hali ambayo matapishi hayo yaliingia katika mirija ya hewa na kuziba hali iliyosababisha kifo chake,” alisema Dk Ngowi.

Alisema hali za majeruhi wengine wanne zinaendelea vizuri, na wanaendelea na mazoezi huku wakila wenyewe hali ambayo wamepanga kesho kuangalia uwezekano wa kuwafanyia vipimo kwa mara nyingine tena.

Aidha, Dk Ngowi alisema endapo hali zao hazitakuwa nzuri na kubadilika, watawahamishia katika Hospitali ya Rufaa kwa ajili ya uangalizi wa juu hali ambayo watapata mabadiliko zaidi ya afya zao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Shigitwa (SHIGOMIKO), Hamza Tandiko alisema wakiwa wachimbaji wadogo wa Mgodi wa Nyangalata wamekipokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mwenzao na kuwataka waliobaki kutokata tamaa Mungu atawasaidia watapata nafuu.

Sisi kama wachimbaji hatupingani na Mwenyezi Mungu tulijitahidi kadri ya uwezo wetu kuokoa maisha yao kwa kushirikiana na uongozi wa Hospitali ya Wilaya, lakini kwa mapenzi ya Mungu ameamua kumchukua Onyiwa akapumzike na hakuna mtu anaweza kuzuia kifo,” alisema Tandiko.

Wachimbaji hao wadogo watano waliokolewa kutoka katika mgodi huo wiki iliyopita baada ya kukaa kwa siku 41 kutokana na kufukiwa na kifusi. Mwenzao mmoja alifia mgodini wakati wakisubiri majaliwa ya kuokolewa.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname