
Aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Mikindani,
mkoani hapa, Hasnein Murji, amesitisha huduma ya usafiri kwa wanafunzi
wa Shule ya Sekondari ya Naliendele kufuatia kushindwa ubunge katika
uchaguzi mkuu wa Oktoba 25.
Murji aligombea jimbo hilo kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Alikuwa akitoa usafiri kwa wanafunzi wa shule hiyo tangu mwaka 2011 alipochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti shuleni
hapo, wanafunzi hao walisema kuwa kitendo cha kutochaguliwa mbunge
huyo kimewaathiri kiusafiri.
‘Tangu alipochaguliwa kuwa mbunge wa
jimbo hili, alitoa magari mawili ambayo yalikuwa yanapokezana, tulikuwa
hatulipi nauli, tulikuwa tunawahi vipindi kwa sababu tulikuwa na uhakika
wa usafiri,’ alisema mmoja wa wanafunzi hao.
Walisema usafiri wa daladala ni mchache, lakini pia wanatozwa nauli ya Sh. 500 badala ya Sh. 200.
Walidai kuwa wakati mwingine wazazi wanashindwa kumudu gharama na kushindwa kufika shuleni kwa sababu ya kukosa nauli.
Walisema hivi sasa wanafunzi wanaofanya
mitihani ya kumaliza kidato cha nne wanalazimika kupanda mabasi ya
Tandahimba na Newala ili kuwahi kufanya mitihani.
Kharim Mohamed, ni mwanafunzi wa kidato
cha tatu, alisema kuwa ukosefu wa usafiri wa uhakika unawafanya
wachelewe vipindi na hukaa kituoni kwa saa tatu wakingoja usafiri.
Awali Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Hittu
Rashid, alisema shule hiyo ilianza mwaka 1997, na tatizo la usafiri kwa
shule hiyo limekuwa la muda mrefu. ‘Miaka ya nyuma kabla sijahamia hapa,
niliambiwa kwamba wanafunzi walikuwa wakitumia malori ya mchanga kama
usafiri wa kuja shuleni, na mwanafunzi mmoja alipata ulemavu baada ya
kuvunjika mguu wakati akipanda gari,’ alisema.
Alisema, tangu kuwepo kwa usafiri wa uhakika wanafunzi wake wamekuwa na mahudhurio mazuri darasani na utoro ukipungua.
‘Kutoka mjini kuja hapa shuleni ni
kilomita 12, na kutokana na tatizo la usafiri kwa wanafunzi wangu
aliyekuwa mbunge aliona tatizo hili akaamua kuwasaidia, zaidi ya
wanafunzi 50 walikuwa wakipanda magari yake bure,’ alisema.
Alipoulizwa na Nipashe kuhusu kusitisha
usafiri huo, Murji, alikiri kuchukua hatua hiyo tangu Jumatatu iliyopita
kwa madai kuwa alikuwa akitoa huduma hiyo kama mbunge wao, lakini sasa
sio mbunge tena ni mfanyabishara kama walivyo wengine.
Aliwataka wamuombe mbunge wao wa sasa awasaidie.
Hata hivyo, alisema atatoa magari kwa
ajili ya kwenda Mikindani kwa wananchi wote na nauli yake itakuwa Sh.
200 bila kujali umri wa mtu.
Akizungumzia mpango wa kuwasaidia
wanafunzi hao hata kwa kuwatoza nauli ili kupunguza makali ya usafiri,
Murji alisema: ‘Kwa kuwa mimi sio mbunge wao tena nafikiria kama
nitaweza huenda nitawapelekea, lakini sijajua itachukua muda gani
kurejesha usafiri shuleni hapo,’ alisema.
Chanzo:Nipashe
No comments:
Post a Comment