JESHI la polisi kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) mkoani Iringa jana
walitumia mabomu ya machozi kuwakamata wafuasi zaidi ya 61 wa chama
cha Demokrasia na maendeleo (chadema ) akiwemo mgombea ubunge wao
jimbo la Iringa mjini mchungaji Peter Msigwa kwa tuhuma za kumpiga
mawe mkuu wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) Iringa na wananchi
waliokuwa wakitoka katika mkutano wa mgombea Urais wa chama cha
mapinduzi (CCM) Dr John Magufuli.
Imeelezwa kuwa wafuasi hao ambao wengi wao ni vijana walikuwa
wamekutana katika eneo la kambi ya kampeni ya Chadema iliyopo eneo
la Hoteli ya Sambala jirani na kambi ya kikosi cha kutuliza ghasia
(FFU) kwa ajili ya kikao cha ndani toka majira ya mchana na jioni
ndipo walipofanya vurugu hizo wakati wananchi wakitoka katika
mkutano wa kampeni za mgombea huyo wa Urais wa CCM.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Ramadhan Mungi amewaeleza
waandishi wa habari kuwa tukio hilo lilitokea jana majira ya saa
12;30 jioni baada ya wafuasi hao kufunga barabara kuu ya Iringa
–Dodoma na kufanya vurugu hizo kwa kuwarushia mawe wananchi
waliokuwa wakitoka katika mkutano wa kampeni za Dr Magufuli uwanja
wa Samora.
Amesema kuwa wakati jeshi la polisi likiwa katika mkutano wa mgombea
huyo wa Urais wa CCM walipokea taarifa kuwa kuna vijana wa boda
boda zaidi ya 150 walikuwa wakijikusanya kuelekea katika eneo hilo
la Sambala Lodge na baada ya kufuatilia ndipo walibaini kuwa
wanakwenda katika kikao chao cha ndani na kwa kawaida jeshi la
polisi halikatazi watu kufanya vikao vyao vya ndani .
“Jeshi la polisi halizuii wanachama wa chama chochote cha siasa
kufanya vikao vya ndani kwani ni haki yao ya kisheria na
kikatiba,lakini baada ya kikao chao kumalizika vijana hao walitoka
nje ya ukumbi huo uliopo kando kando ya barabara na kuanza kufunga
barabara na kucheza muziki katikakati ya barabara na kuzuia watumiaji
wengine wa barabara
"Baada ya vurugu hizo nilimuagiza mkuu wa FFU kwenda kuwatoa watu
hao barabarani ila walipuuza na kuishia kumpiga mawe na baadae
kukimbilia kujifungia katika Lodge hiyo ya Sambala eneo ambalo
wamefanya kama makao makuu ya Kampeni za Chadema “ alisema kamanda
Mungi.
Amesema wakati wa vurugu hizo baadhi ya vijana waliumia kwa kuruka
ukuta na wengine kwa kuanguka wakati wakijaribu kukwepa kukamatwa na
kuwa wale wote waliokamatwa watafikishwa mahakamani wakati wowote
kuanzia sasa na kuwa miongoni mwao yumo mgombea ubunge jimbo
hilo,Mchungaji Msigwa .
Mbali ya mchangaji Msigwa wengine waliokamatwa kwa tuhuma za
vurugu hizo ni pamoja na mgombea udiwani kata ya Gangilonga ambae
pia ni mkuu wa kambi hiyo Dady Igogo
Hata hivyo, taarifa iliyotufikia jion hii inaarifu kuwa Mchungaji Msigwa na wafuasi hao 61 wameachiwa kwa dhamana leo.
No comments:
Post a Comment