25 September 2015

MAHUJAJI WA 5 KUTOKEA TANZANIA WATHIBITISHWA KUFA HUKO MAKKA

WATU wasiopungua 700 wamekufa, huku wengine 816 wakijeruhiwa jana jirani na mji Mtakatifu wa Makka walikokwenda kuhiji ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa moja ya nguzo muhimu katika Imani ya dini ya Kiislamu.Kwa mujibu wa Baraza la Taasisi na Jumuiya za Kiiislam nchini, kati ya mahujaji 2,000,000 waliokwenda Saudi Arabia mwaka huu, 1,500 wanatoka Tanzania.Kwa mujibu wa taarifa ya Sheikh Abu Bakari Zuberi Mufti wa Tanzania,  kwa vyombo vya habari amesema tayari wamethibitisha kutokea vifo vya watu watano waliotokea Tanzania miongoni mwao mmoja ni raia wa Kenya na wengine  wanne ni Watanzania.Amesema Watanzania waliotambuliwa hadi jana usiku wametajwa kuwa ni, Mwanaisha Hassan Juma, Mkungwe Suleiman Hemedi na Sefu Saidi Kitimla. Mwanamke mwingine mmoja Mtanzania jina halijaweza kupatikana hadi Alhamisi usiku wakati wakiandaa taarifa hii ambapo raia wa Kenya ametambuliwa kwa jina la Fatuma Mohammed Jama.Kuna taarifa ya mahujaji wanawake wawili ambao hadi Septemba 24, 2015 usiku walikua hawajapatikana hivyo hawakuwa na uhakika juu ya usalama wao hadi watakapoonekana ama kupata taarifa zao.Kwa mujibu wa Mufti Zuberi, majina ya marehemu hao yamepatikana kupitia vitambulisho vyao ambavyo wahanga wa tukio hilo waliweza kuvichukua kutoka kwenye miili ya marehemu.
Ameeleza kuwa amepokea taarifa za majeruhi miongoni mwa mahujaji wa Tanzania na baadhi ya majeruhi hao ameonana nao mara baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini.
Vilevile ameagiza maafisa wa Bakwata alioko nao Mina kuendelea kufuatilia habari na taarifa za mahujaji wengine wa Tanzania katika hospitali na sehemu za kuhifadhia maiti, ili aweze kuwa na uhakika juu ya usalama wa mahujaji waliotokea Tanzania.
Katika kipindi hiki cha taharuki kubwa amesema wanafanya mawasiliano na Wizara husika huko Saudi Arabia kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia ubalozi wake wa Saudi Arabia ili mkanganyiko wa taarifa ambazo zinazidisha taharuki kwa ndugu na jamaa wa mahujaji zisiendelee kuwaweka katika wakati mgumu.
Amewaomba ndugu na jamaa wa mahujaji kuwa watulivu na kuwa na subra katika wakati huu mgumu kwa watu wengi, kwani wanaendelea kufuatilia kwa karibu sana tukio hilo na mara wakipata taarifa za uhakika watatoa taarifa zaidi.
Hata hivyo,amesema kutokana na idadi ya maiti kuwa kubwa serikali ya Saudi Arabia wanaendelea na zoezi la kutambua uraia wa kila mwili ili waweze kutoa taarifa zaidi na wanatarajia wakati wowote watakuwa wamepata taarifa zaidi.
CHANZO FIKRA PEVU

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname