Spika wa Bunge, Anna Makinda, amewataka wakazi wa mikoa ya Nyanda za
Juu Kusini kuepuka wagombea watakaowashawishi kwa kuwapa rushwa ili
wachaguliwe wakati Uchaguzi Mkuu nchini Oktoba 25, mwaka huu kwa sababu
wanachangia kukithiri umaskini nchini.
Makinda alitoa kauli hiyo juzi, wakati akifungua Maonyesho ya 23 ya
Kilimo maarufu kama Nanane Kanda hiyo yanayofanyika viwanja vya John
Mwakangale vilivyopo nje kidogo ya Halmadhauri ya Jiji la Mbeya.
Alisema wakazi wa mikoa ya kanda hiyo ya Mbeya, Iringa, Njombe, Ruvuma,
Songwe na Rukwa, jukumu kubwa lao kubwa ni kuchagua kiongozi bora na
kuwakwepa watoa rushwa.
Alisema rushwa katika uchaguzi ina madhara makubwa kwa sababu kwa
kiwango kikubwa inayochangia kukithiri kwa umaskini katika jamii.
" Nasema hivi wakileta pokeeni na kura msiwapigie, "alisisitiza.
Kwa upande mwingine aliwahamisha wakazi hao kutumia fursa ya Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa Songwe (SIA) kuongeza uzalishaji mazao ya chakula na
biashara na kujiongezea kipato.
Makinda alisema serikali imewekeza kwa kuboresha miundombinu ya barabara
na anga kwa ajili ya kuwatengenezea mazingira wakulima ya kupata soko
la uhakika la mazao na kukuza uchumi na pato la taifa.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Saidi Mwambungu, alisema serikali
imeweka mikakati ya kupatikana kwa masoko ya mazao ya wakulima na
kuwataka wakuu wa mikoa hiyo na halmashauri nchini kuhakikisha maofisa
ugani wanakwenda vijijini kutoa elimu ya kilimo bora kwa wakulima.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment