Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimeshika nafasi ya kumi miongoni mwa vyuo vikuu 50 bora na vyenye umaarufu Afrika.
Kadhalika UDSM kimetajwa kuwa miongoni mwa chuo vikuu chenye idadi kubwa ya wanafunzi na walimu na wingi wa programu za masomo.
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala alisema chuo hicho
kina haki ya kushika nafasi hiyo kutokana na jitihada zinazofanywa na
uongozi.
“Tulifanya jitihada kuhakikisha tuna walimu wazuri wenye shahada za
uzamili na uzamivu, maabara nzuri na miundombinu rafiki ya kufundishia,”
alisema Mukandala.
Alisema UDSM ina mitaala bora inayoendana na wakati na inazalisha wataalamu wengi kwa mwaka.
“UDSM inachaguliwa na wanafunzi wengi na pia ina wanafunzi wa kimataifa,”alisema.
Katika matokeo ya utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Kimataifa ya Vyuo
Vikuu na vya Kati (4ICU) ya Uingereza, chuo hicho kilishika nafasi ya
10 kati ya vyuo 50 vilivyopimwa kulingana na vigezo vya taasisi hiyo.
Hata hivyo, taasisi hiyo ilieleza kuwa hawapimi ubora wa vyuo kwa
kuangalia kiwango cha elimu inayotolewa au huduma bali wanaangalia
umaarufu wa chuo kimataifa.
“Huu mtandao si kwa ajili ya taaluma wala usichukuliwe kama kipimo cha
kuchagua programu au nafasi ya masomo, huu ni kwa ajili ya kuwasaidia
wanafunzi wa kimataifa kufahamu jinsi taasisi ya elimu ilivyo maarufu
katika nchi nyingine,” ilisema taarifa ya 4ICU.
Katika taarifa hiyo, Chuo Kikuu cha Cape Town cha Afrika Kusini
kilishika nafasi ya kwanza huku vingine vilivyoshika tano bora vikitoka
nchini humo.
Nafasi ya pili ilishikwa na Chuo Kikuu cha Pretoria, ya tatu Chuo Kikuu
cha Stellenbosch na nne ilikwenda kwa Chuo Kikuu cha Witwatersand na
tano ikishikwa na Chuo Kikuu cha Afrika Kusini.
Ikieleza namna walivyoweza kupata vyuo bora, tovuti ya 4ICU iliangalia
jinsi mitandao mingine inavyozungumza na kutoa taarifa za chuo husika,
nafasi yake katika kurasa za mtandao ya kijamii kutafuta taarifa kwa
google, chuo kinavyotumiwa kama rejea katika taarifa mbalimbali na ni
kwa kiasi gani watu wanaitumia tovuti ya chuo husika

No comments:
Post a Comment